Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .MKUTANO wa 28 wa Kamati ya Viwango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika mkoani Arusha, ukilenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika maeneo ya uandaaji wa viwango, ukaguzi wa ubora, vipimo na uthibitishaji.
Aidha mkutano huo unaofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzia Mei 12 hadi 14, 2026, umewakutanisha wataalamu kutoka nchi wanachama wa EAC, kamati ndogo za kitaalamu, taasisi za viwango pamoja na washirika wa maendeleo kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha biashara ndani ya ukanda huo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwakilishi wa Shirika la Viwango Tanzania, Davidi Lema, amesema kamati hiyo ni chombo cha kisheria kilichoanzishwa chini ya sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuratibu na kufuatilia shughuli za viwango, ukaguzi wa ubora, vipimo pamoja na uthibitishaji wa bidhaa na huduma.
Amesema lengo kuu la kamati hiyo ni kuhakikisha biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea kukua kwa kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyoweza kuchelewesha usafirishaji wa bidhaa na huduma kati ya nchi wanachama.
“Tunataka kuwa na mfumo mmoja wa viwango utakaorahisisha biashara, kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika Mashariki na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika ukanda wetu zinakidhi ubora unaokubalika kimataifa,” amesema Lema.
Ameongeza kuwa mkutano huo pia umejadili maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya viwango na ubora, pamoja na kuweka vipaumbele vya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa lengo la kuimarisha sekta ya viwanda na biashara ndani ya EAC.
“ushirikiano huo wa kikanda utasaidia kuongeza ufanisi wa mifumo ya vipimo na uthibitishaji wa bidhaa, kulinda afya na usalama wa walaji, pamoja na kufungua fursa zaidi za biashara ndani na nje ya Afrika Mashariki.”amesema Lema .
Mkutano huo unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Jumuiya ya Afrika Mashariki za kuimarisha mtangamano wa kiuchumi kwa kutumia viwango vya pamoja vitakavyosaidia kukuza ushindani wa bidhaa na huduma katika soko la kikanda na kimataifa.
Naye Afisa viwango kutoka TBS ,Mary Ottaru amesema kuwa,lengo la kuwakutanisha wadau hao ni kuhakikisha bidhaa zao wanazozalisha zinakidhi matakwa ya viwango na usalama na bidhaa wanazotumia zinakuwa na alama bora ya TBS ili kuwa na usalama wa bidhaa na kulinda afya zao.
“Tunatoa wito kwa wadau hao kuhakikisha wanatumia bidhaa ambazo zimedhibitishwa na TBS kwa ajili ya usalama wao na wananchi kwa ujumla .”amesema Mary.

