*Mazungumzo na Mwekezaji Yamefikia Zaidi ya Asilimia 90
*Kuzalisha Tani Milioni 2.9 za Chuma Ghafi kwa Mwaka
*Kuzalisha Ajira Rasmi 6,500, Zisizo Rasmi 26,000
Njombe
Serikali ya Tanzania ndani ya kipindi cha Miezi Mitatu ijayo inatarajiwa kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Liganga na Mchuchuma wenye uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 2 hadi 3 baada ya mazungumzo kati ya Serikali na Mwekezaji kufikia zaidi ya asilimia 90.
Hayo yalibainishwa Mei 9, 2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Shamba la Parachichi la Havira Farm Mkoani Njombe, pembeni mwa Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini, kinachotumika kama sehemu ya tathmini na kujipanga.
Alisema hatua hiyo inaashiria mwanzo wa utekelezaji wa mradi huo uliosubiriwa kwa miaka mingi ukitarajiwa kuongeza mapato ya Seikali, ajira kwa wananchi, kukuza sekta ya viwanda vya chuma na ustawi wa jamii inayozunguka mradi na taifa.
Aliongeza kwamba, mradi huo unatarajiwa kuzalisha tani milioni 2.9 za chuma ghafi kwa mwaka pamoja na tani milioni 1.1 za bidhaa za chuma kwa mwaka, huku ukitarajiwa kutoa zaidi ya ajira rasmi 6,500 na ajira zisizo rasmi zipatazo 26,000
‘’ Katika kipindi cha miaka 25 ya kwanza ya mradi, jumla ya mapato ya dola za Marekani 1,990,489,585,000 zinatarajiwa kupatikana ambapo kwenye miradi ya makaa ya mawe kiasi cha dola za Marekani 92,593,820; uchimbaji chuma kiasi cha dola za Marekani 910,781,519 na kiwanda cha chuma kiasi cha dola za Marekani 987,114,246,’’ alisema Msigwa.
Pia, aliongeza kwamba utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa msongo wa umeme wa Kilovoti 220 kati ya mchuchuma na na liganga na barabara kutoka Mchuchuma na Liganga ukiwemo mgodi wa makaa ya mawe mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 3 kwa mwaka na Kituo cha kufua umeme kwa megawati 600.
Msigwa alisema tayari Serikali imelipa zaidi ya shilingi bilioni 15 za fidia kwa wananchi ili kupisha utekelezaji wa mradi huo, hatua inayoonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha mradi huo unaanza kwa vitendo baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu.
Utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma unaashiria safari ya kuelekea Dira 2050 ambapo kupitia Sekta ya Madini imejipanga kufikia Uchumi wa Dola trilioni Moja ukiwa ni miongoni mwa miradi kielelezo iliyoanishwa kwenye mpango wa muda mrefu wa wa dira hiyo unaotarajiwa kuchochea sekta ya viwanda nchini.
Mbali na Sekta ya Madini, alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Njombe ikiwemo barabara, maji na umeme kwa lengo la kuufungua zaidi mkoa huo kiuchumi na kijamii.

