MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,akiwahutubia wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba katika mwendelezo wa ziara zake za kuimarisha chama na kuwashukru wanachama wa chama hicho baada ya kushinda uchaguzi mwaka 2025, mkutano huo umefanyika ukumbi wa Hijazi Complex Wilaya ya Mkoani Pemba.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Mohamed Said Dimwa,akitoa salamu za CCM katika ziara ya Makamu Mwenyekiti Dk.Hussein Mwinyi,huko Wilaya ya Mkoani Pemba iliyofanyika leo tarehe 13/05/2026.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,akikata utepe wa kuzindua ukumbi wa CCM Hijazi Complex kabla ya kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba.
………….
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amezitaka Kamati za Maadili za CCM kuanzia ngazi ya matawi hadi taifa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuepusha malalamiko ya kuonewa kwa baadhi ya wanachama wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa uchaguzi.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo katika mwendelezo wa ziara zake za kuimarisha Chama, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Pemba na wilaya zake katika Ukumbi wa Hijazi Complex, Tawi la CCM Ng’ombeni, Wilaya ya Mkoani, Pemba.
Alisema Kamati za Maadili zina wajibu wa kufuatilia mienendo ya wanachama na viongozi kwa kila ngazi pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba, kanuni na miongozo ya Chama.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa baadhi ya kamati hizo zimekuwa zikishindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati, hali inayosababisha hatua kuchukuliwa pale mwanachama anapotangaza nia ya kugombea nafasi ya uongozi.
“Kamati za maadili tekelezeni wajibu wenu ipasavyo ili kuepusha malalamiko na migogoro isiyokuwa ya lazima ndani ya Chama na Jumuiya zake. Si sahihi kusubiri mwanachama anapotaka kugombea ndipo awekewe pingamizi, wakati taratibu za kinidhamu kama onyo, karipio na onyo kali zipo,” alisema Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa kuchukua hatua mapema dhidi ya mwanachama anayekiuka maadili kunasaidia kuondoa malalamiko na sintofahamu kabla ya mchakato wa uchaguzi.
Aidha, alisema mkutano huo ulikuwa na lengo la kuwashukuru viongozi wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba kwa mchango wao mkubwa uliokisaidia Chama kupata ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Dk. Mwinyi aliwataka viongozi wa CCM kujipanga kisaikolojia kuelekea uchaguzi wa ndani wa Chama mwaka 2027, akieleza kuwa uzoefu unaonesha kuwepo kwa makundi na safu zisizofaa zinazoundwa kwa maslahi binafsi katika kipindi hicho.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema CCM itaendelea kutekeleza ahadi zake za uchaguzi kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba na maeneo jirani.
Pia aliahidi kuwasilisha mapendekezo Makao Makuu ya CCM kuhusu kuboreshwa kwa maslahi ya watumishi wa Chama na Jumuiya zake ili yaendane na watumishi wa Serikali.
Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kufufuliwa na kuimarishwa kwa Kamati za Maadili ili zifanye kazi zake kwa ufanisi katika ngazi zote za Chama, badala ya kusubiri kipindi cha uchaguzi.
Alisema CCM ilipata ushindi wa zaidi ya asilimia 75 katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, jambo alilosema ni mafanikio makubwa ya kisiasa yaliyopatikana katika mazingira ya amani na utulivu.
Akijibu hoja kuhusu ujenzi wa barabara ya Mkoani kwenda Chakechake, alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha masharti ya wahisani wa maendeleo, ikiwemo masuala ya fidia na tathmini ya mazingira, ili ujenzi huo uanze wakati wowote.
Akitoa salamu za Chama, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohamed Said Dimwa, alisema mafanikio ya maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar yanatokana na usimamizi mzuri wa sera za CCM.
Dk. Dimwa alisema CCM imeendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wananchi na Serikali katika kuharakisha maendeleo mijini na vijijini.
“Wananchi wa Wilaya ya Mkoani wanaendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, vikundi vya ujasiriamali, uvuvi wa kisasa pamoja na kuimarishwa kwa kilimo cha karafuu kupitia sera madhubuti za CCM,” alisema Dk. Dimwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma, aliomba kuboreshwa kwa maslahi ya watumishi wa Chama na Jumuiya zake pamoja na kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto ya ubovu wa barabara ya Mkoani kwenda Chakechake.
Aidha, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuahidi kuwa wanachama wa Mkoa huo wataendelea kumuunga mkono pamoja na kuhakikisha Chama kinaendelea kupata ushindi katika chaguzi zijazo.
Katika ziara hiyo, Dk. Mwinyi alizindua Ukumbi wa Kisasa wa Hijazi Complex uliopo Tawi la CCM Ng’ombeni, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, ambao umejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 280.
