Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akijibu maswali katika kikao cha 28 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge jijini Dodoma leo Mei 13, 2026

………

Serikali imesema mchakato wa kuliimarisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kulipandisha hadhi kuwa Mamlaka ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, upo katika hatua za maamuzi.

Imesema hatua hiyo italiwezesha Baraza hilo kuwa chombo madhubuti na taasisi mahiri ya usimamizi na utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa bungeni jijini Dodoma leo Mei 13, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Shaurimoyo Mhe. Mattar Ali Salumu aliyeuliza kwanini Serikali haipandishi hadhi NEMC kuwa Mamlaka ili iweze kufanya majukumu yake kwa ufanisi.

Akijibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa alifafanua kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 kwa kuzingatia haja ya kuimarisha uwezo wa taasisi katika usimamizi na utekelezaji wa sheria hiyo na kuongeza ufanisi wa kiutendaji wa Baraza katika majukumu yake.

Alisema kuwa Serikali inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuliwasilisha bungeni suala hilo la kuifanya nemc kuwa mamlaka kamili baada ya kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya Serikali katika maandalizi ya awali.

“Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya kazi kwa ukaribu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha kwamba maandalizi ya muswada huo utakaokuja bungeni yawe yamezingatia vitu vyote vya msingi, alisisitiza Mhe. Kwagilwa.

Aidha, Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na NEMC inaendelea na maandalizi ya Waraka wa Baraza la Mawaziri ambapo kikao kazi cha kukamilisha waraka huo kinatarajiwa kufanyika Mei 14, 2026.

Miongoni mwa yaliyozingatiwa katika hatua za awali ni pamoja na mapendekezo ya marekebisho ya vifungu vya sheria vilivyoanzisha Baraza na majukumu yake ili viweze kuanzisha Mamlaka.

Halikadhalika, masuala mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na kubainisha majukumu yake pamoja na muundo na majukumu ya Bodi kwa mujibu wa mfumo mpya unaopendekezwa.