Na Silivia Amandius,
Karagwe.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanza rasmi kutekeleza zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka, kufuatia maagizo yaliyotolewa Mei 9, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratias Ndejembi, wakati wa ziara yake mkoani Kagera.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi la ulipaji fidia may 12, mwaka huu ikiwa ni Moja ya maagizo ya waziri wa nishati katika Kata ya Nyakahanga, wilayani Karagwe, Mhandisi Mpima Ardhi wa mradi huo kutoka makao makuu ya TANESCO, Eng. Derick Kaijanangoma, amesema jumla ya shilingi bilioni 1.7 zimetengwa kwa ajili ya ulipaji fidia katika awamu ya kwanza.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika halmashauri nne za mkoa wa Kagera na unatarajiwa kunufaisha wananchi 280 kutoka kata 3, huku zoezi la tathmini ya mali za wananchi likiwa lilianza tangu mwaka 2022.
“Zoezi la ulipaji fidia tayari limefanyika katika wilaya ya Ngara na sasa linaendelea katika maeneo ya Karagwe. Tunawasihi wananchi kutumia vyema fedha wanazolipwa ili kuepuka migogoro ya kifamilia na ardhi,” amesema Eng. Kaijanangoma.
Amebainisha kuwa baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni pamoja na migogoro ya umiliki wa ardhi na baadhi ya wananchi kukimbia familia zao, hali inayoweza kuathiri utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, ameeleza kuwa baada ya kulipwa fidia, wananchi hawataruhusiwa kuendelea kufanya shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mradi, na wametakiwa kuondoa mali zao ndani ya siku 30, huku uwezekano wa kuongezewa muda ukiwepo pale inapobidi ili kumpa nafasi mkandarasi kuendelea na kazi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi akiwemo mkazi wa Kijiji cha Bisheshe, ndg. Fidelix Kajunangoma wameishukuru serikali na TANESCO kwa kuanza kulipa fidia, licha ya kuchelewa kwake.
“Tunalishukuru shirika kwa kutulipa fidia. Ingawa imechelewa, tuko tayari kupisha mradi huu kwa manufaa ya wananchi wengine ambao bado hawajapata huduma ya umeme,” amesema mmoja wa wananchi hao.
Mradi huo wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

