Na Aisha Swahibu, WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuboresha huduma za dharura nchini kwa kuongeza idadi ya wodi za huduma hizo kutoka wodi saba mwaka 2021 hadi kufikia wodi 125 Machi 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuokoa maisha ya Watanzania.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, wakati akijibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa wabunge kuhusu utekelezaji wa huduma za afya ,leo Mei 12, 2026, bungeni jijini Dodoma.

Dkt. Flerence amesema kuwa huduma za dharura hutolewa kwa mgonjwa anayefika hospitalini ndani ya saa moja, ambapo huduma anazopatiwa hulenga kuokoa maisha yake kwa asilimia kubwa kupitia utoaji wa huduma zote za msingi zinazohitajika kwa wakati.

Aidha, Serikali imeongeza idadi ya magari ya kubebea wagonjwa wa dharura ( Ambulence) kutoka magari 540 mwaka 2021 hadi kufikia magari 1,267 mwezi Machi 2026. Vilevile, Serikali imenunua boti saba kwa ajili ya maeneo yaliyozungukwa na maji pamoja na pikipiki 300 zilizogawiwa katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kuimarisha huduma za chanjo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amemshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani ya kumteua na kuahidi kuitumikia kwa heshima na hekima kazi hiyo kwa maslahi ya watanzania huku akimpa pongezi Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kazi kubwa na misimamo pamoja na uongozi wake wa kusimamia vyema Wizara hiyo.