Na Mwandishi wetu, Babati
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege amekabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa hospitali na chuo cha uuguzi Dareda cha Wilayani Babati mkoani Manyara.
Pia, Naibu Waziri Ndege amewatembelea wagonjwa wakiwemo watoto na wanawake waliojifungua kwenye hospitali ya Dareda taasisi inayomiliwa na Jimbo Katoliki la Mbulu na kuwapa mahitaji mbalimbali.
Naibu Waziri Ndege ambaye pia ni mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara, amekabidhi mifuko hiyo 100 ya saruji na mahitaji mbalimbali ya wagonjwa kwenye hospitali hiyo.
Mahitaji aliyotoa hospitalini hapo kwa wagonjwa hao ni pamoja na taulo za kike, sabuni, sukari, mafuta ya kujipaka, sharubati na taulo za watoto wadogo (pampas).
Akizungumza kwenye tukio hilo Naibu Waziri Ndege amesema watumishi wa hospitali hiyo wakiwemo madaktari na wauguzi wamekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wagonjwa ipasavyo.
“Nimeridhishwa na huduma zinazotolewa na madaktari na wauguzi wa hospitali hii hivyo wananchi tuendelee kuwapa ushirikiano wahudumu wa afya,” amesema Naibu Waziri Ndege.
Amesema kazi ya utoaji huduma za afya ni kazi ya kujitolea kwa jamii na kuhitaji kupewa moyo na kujitoa kwa hali ya juu katika kuhudumia na kutibu jamii.
Amewapongeza manesi na madaktari kwa juhudi wanazozifanya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, huku akieleza kuwa aliona ni vyema kuwapa salamu na msaada mdogo akina mama pamoja na watoto waliolazwa hospitalini hapo.
“Pokeeni zawadi hiyo niliyotoa kwa ajili ya hospitali hii na wagonjwa mpokee hicho kidogo tulichogawana na ninawaombea afya njema na mpate nguvu,” amesema Naibu Waziri Ndege.
Diwani wa kata ya Dareda, Willbroad Bayo amemshukuru Naibu Waziri Ndege kwa kujitolea huko kwani mifuko hiyo 100 ya saruji itasaidia ujenzi wa taasisi hiyo ya hospitali ya Dareda.
“Hakika tunampongeza sanaa kwa jinsi alivyo jitolea kwa hali na mali,
mhe Regina kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa hospitali na jengo la chuo cha Dareda nursing, aksante sana mheshimiwa Naibu Waziri, hakika umetuunga mkono pakubwa sana,” amesema Bayo.
Mkazi wa kata ya Dareda, Magdalena Tsere ametoa shukurani za dhati kwa Naibu waziri Ndege kwa kukabidhi mifuko hiyo 100 ya saruji kwa ajili ya kuzungushia ukuta.
Tsere amesema Naibu waziri Ndege ambaye pia ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Manyara, amekuwa mfano bora kwa viongozi ambao wanajali jamii inayomzunguka.
