Na Fullshangwe Blog,Dodoma
WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha wanawalea watoto katika maadili mema pamoja na kuwapeleka shule kwa wakati ili kuwaandaa kuwa wananchi wenye nidhamu, maarifa na mchango chanya kwa taifa.
Wito huo umetolewa leo Mei 9, 2026 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dodoma, Samwel Malechelawakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kimkoa yaliyofanyika katika Kata ya Mpunguzi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Malechela alisema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na elimu, akieleza kuwa hayo ndiyo msingi wa maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
“Mzazi anatakiwa kuwa karibu na mtoto wake muda wote, kumfundisha maadili mema na kuhakikisha anapata haki yake ya elimu. Tusiposhirikiana na walimu tutashindwa kupambana na changamoto ya utoro shuleni,” alisema Malechela.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, walimu na viongozi wa jamii katika kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo kikamilifu na kufikia ndoto zao za maisha.
Alibainisha kuwa baadhi ya watoto hukosa mwongozo mzuri kutokana na wazazi kutokuwa karibu nao jambo linalochangia kushuka kwa ufaulu na kuongezeka kwa vitendo visivyofaa katika jamii.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Rozalia Hhari aliwahimiza wazazi kushiriki kikamilifu katika kutokomeza tatizo la utoro kwa kuwafuatilia watoto wao mara kwa mara na kushirikiana na walimu kufahamu maendeleo yao kitaaluma na kitabia.
“Ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha mtoto anafika shule na anabaki katika mazingira mazuri ya kujifunza. Tukiwa na mshikamano kati ya familia na shule tutafanikiwa kujenga kizazi chenye maadili na elimu bora,” alisema Hhari.
Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwataka wananchi wa Mpunguzi kutunza ardhi yao huku wakihimizwa kutouza mashamba kiholela kutokana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma na kupanda kwa thamani ya viwanja.
“Acheni kuuza mashamba na kuhama mbali. Ni lazima wenyeji wabaki na kufaidika na maendeleo ya eneo lao,” ilisisitizwa katika maadhimisho hayo.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Dodoma Mjini, Stephene Mwanga alisema jumuiya hiyo imeendelea kuisimamia serikali kwa karibu kwa kufanya ziara katika kata zote 41 za wilaya hiyo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Mwanga alitoa mfano wa Kata ya Chigongwe ambapo walikuta pampu ya maji imeibiwa na kuuzwa Kahama kabla ya kukamatwa na kesi kufikishwa Mahakama ya Mwanzo Chamwino.
“Sisi kama Jumuiya ya Wazazi tuliona wananchi wanahitaji huduma ya maji haraka, hivyo tulishirikiana kuhakikisha pampu inarudishwa ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji,” alisema Mwanga.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mpunguzi, Isaya Chilongani alisema kata hiyo imeendelea kunufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nkulabi ambapo zaidi ya shilingi milioni 46 zilitolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya ujenzi huo, huku wanafunzi tayari wakianza kutumia madarasa hayo.
Pia alieleza kuhusu mradi wa ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Nkulabi ulioanza kwa nguvu za wananchi kabla ya kupata ufadhili zaidi kutoka kwa wadau wa maendeleo na serikali, ambapo jumla ya shilingi milioni 18 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo.
Maadhimisho hayo ya Wiki ya Wazazi Kimkoa yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wazazi, viongozi na wananchi kujadili masuala ya malezi, elimu na maendeleo ya jamii, sambamba na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata ya Mpunguzi.

