Angela Jasmine Mbelwa Kairuki Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amewataka wanawake nchini kuweka mkazo katika malezi bora ya watoto pamoja na kulinda afya zao ili kujenga kizazi chenye maadili, afya njema na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.

Waziri Kairuki aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Wanawake na Biashara lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, ambapo alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio ya biashara, uongozi na maendeleo ya kiuchumi, bado familia na malezi ndiyo msingi wa ustawi wa jamii.

Amesema wanawake wana nafasi kubwa katika kujenga maadili ya familia na taifa kwa ujumla, hivyo wanapaswa kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama yenye upendo, mafunzo mazuri na uangalizi wa karibu kuanzia wakiwa wadogo.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki aliwataka wazazi kusimamia matumizi ya simu na mitandao ya kijamii kwa watoto wao, akisisitiza kuwa teknolojia inapaswa kutumika kwa manufaa ya elimu, biashara na maendeleo badala ya kuharibu maadili ya jamii.

Alisema wazazi wengi wamekuwa wakiwaachia watoto uhuru mkubwa wa kutumia simu na mitandao bila uangalizi, jambo linalochangia watoto kuathirika kimaadili na kisaikolojia kutokana na maudhui yasiyofaa wanayokutana nayo mtandaoni.

Aidha, Waziri huyo alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, yakiwemo matusi, udhalilishaji na usambazaji wa taarifa zisizofaa, ni kosa kisheria na Serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wahusika ili kulinda maadili ya jamii na usalama wa watoto.

Katika kongamano hilo, Garvin Kweka ambaye ni daktari bingwa wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, alitoa elimu kuhusu afya ya akili, lishe na athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa wanawake na watoto.

Daktari Kweka alivunja ukimya kuhusu madhara ya matumizi ya shisha pamoja na kutotumika vizuri kwa dawa aina ya folic acid kwa wanawake wajawazito, akisema hali hiyo imekuwa chanzo cha watoto kuzaliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo mapungufu ya akili na ukuaji usio wa kawaida wa kichwa.

Alisema matumizi ya shisha kwa watoto wa kike na wanawake wenye umri mdogo yameongezeka kwa kiwango kinachotia wasiwasi, huku akieleza kuwa kemikali zinazopatikana kwenye shisha zinaweza kuathiri mfumo wa fahamu na afya ya uzazi kwa mwanamke.

Kwa mujibu wa Daktari Kweka, wanawake wengi wamekuwa wakipuuza matumizi sahihi ya dawa aina ya folic acid wakati wa ujauzito jambo ambalo linaweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto tangu akiwa tumboni.

Alifafanua kuwa folic acid ni kirutubisho muhimu kinachosaidia ukuaji wa mfumo wa fahamu wa mtoto na kupunguza hatari ya mtoto kuzaliwa na matatizo ya ubongo pamoja na uti wa mgongo.

Aidha, aliwataka wanawake kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na kujiepusha na matumizi ya vileo, sigara, shisha pamoja na dawa za kulevya ili kuhakikisha watoto wanazaliwa salama na wenye afya njema.

Daktari Kweka pia aligusia ongezeko la changamoto za afya ya akili katika jamii, akisema msongo wa mawazo, matumizi ya dawa za kulevya na ukosefu wa malezi bora vimekuwa vikichangia vijana wengi kushindwa kuhimili changamoto za maisha.

Alisema baadhi ya dalili za changamoto ya afya ya akili ni pamoja na kupoteza kumbukumbu, kukosa utulivu wa akili, maumivu ya kichwa ya mara kwa mara pamoja na mabadiliko ya kitabia yanayoweza kuathiri mahusiano na maisha ya kila siku.

Wakati hayo yakielezwa,imekumbushwa kuwa Tanzania ilipiga marufuku matumizi ya shisha zaidi ya miaka 10 iliyopita kutokana na madhara yake kwa afya ya jamii, hususan kwa vijana na wanawake.