Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally Kakurwa amesema zaidi ya Watanzania milioni sita wanajishughulisha na shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya uvuvi katika mnyororo wa thamani, hatua inayoonesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa wananchi.

Akizungumza Mei 9, 2026 wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Waziri Bashiru amesema sekta ya uvuvi imetoa ajira kwa wavuvi 201,661 pamoja na wakuzaji viumbe maji 49,084 nchini.

Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa bajeti ya wizara kwa zaidi ya asilimia 85 kutoka shilingi bilioni 295.92 mwaka 2024/2025 hadi kufikia shilingi bilioni 460 mwaka 2025/2026, jambo lililowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupanua utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika sekta ya mifugo, Waziri Bashiru amesema serikali inaendelea kutekeleza kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo pamoja na miradi mbalimbali ikiwemo mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi, mradi wa vijana wa uzalishaji wa malisho na unenepeshaji wa mbuzi-Kongwa pamoja na kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa malisho ya mifugo.

Amesema Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu kilichoundwa chini ya Sheria ya Mashauriano katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2003 kwa lengo la kuwashirikisha wafanyakazi katika kuboresha mipango, usimamizi na utekelezaji wa shughuli za serikali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Agnes K. Meena amesema Baraza hilo limeundwa mwaka 2025 kufuatia kuunganishwa kwa sekta ya mifugo na uvuvi ambapo awali kulikuwa na mabaraza mawili tofauti yaani Baraza la Mifugo na Baraza la Uvuvi.

Amesema Baraza hilo lina wajumbe 95 na lina jukumu la kuishauri wizara kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika utekelezaji wa shughuli zake, ili kuendeleza. Sekta ya mifugo na uvuvi.

Naye Samweli Nyugwa mwakili wa Katibu Mkuu kutoka TUGHE, amepongeza kuundwa kwa Baraza hilo akisema ni utekelezaji wa takwa la kisheria, na ni. chombo muhimu katika mawasiliano na utatuzi wa changamoto kwa kuwashirikisha wafanyakazi ili kuongeza tija katika utendaji kazi.

Kwa ujumla, Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha sekta za mifugo na uvuvi kupitia ongezeko la bajeti, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika kuboresha utoaji wa huduma, hatua hizo zinatajwa kuwa chachu ya kuongeza ajira, kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha mchango wa sekta hizo katika maendeleo ya taifa.