Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akizungumza na mwananchi wa kata ya Ilemba.

 Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ilemba. 

…………. 

Na Neema Mtuka Sumbawanga

Rukwa :Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile amewataka watendaji kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali inayofika kwenye maeneo yao.

Nyakia amesema hayo katika mkutano wa hadhara alioufanya katika kijiji cha Ilemba kata ya Ilemba halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na kutatua mgogoro kati ya wananchi na tume ya umwagiliaji.

Nyakia amesema makubaliano yaliyokuwepo baina ya wananchi na tume hiyo yafanyiwe kazi na pande zote na yeye hawezi kuingilia makubaliano hayo isipokuwa ana shauri.

” Siwezi kuvunja makubaliano yenu bali yale yote mliyokubaliana ndiyo yatendeke na si vinginevyo ” amesema Nyakia.

Baadhi ya Wananchi akiwemo Shija Melimeli amesema walikuwa na makubaliano na tume ya umwagiliaji kulipia gunia moja la mpunga lakini wanashangaa kuona wanadaiwa magunia mawili ambayo ni kinyume na makubaliano.

“Tume ya umwagiliaji ilikuja na tulikubaliana kila mkulima kuchangia gunia moja la mpunga kwa heka moja lakini makubaliano hayo yamekiukwa” amesema Shija.

Ndipo mkuu wa wilaya ya Sumbawanga akawataka watendaji kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kutoa namba maalum ambayo wakulima watatuma pesa na kuachana na mfumo wa kuchangia gunia moja la mpunga.

Kwa upande wake mhandisi wa umwagiliaji mkoa wa Rukwa mha.Lukas Maganga amewataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi ambacho serikali ina shughulikia changamoto hiyo.

Hali hiyo ya sintofahamu ilitokana na mfereji unaopitisha maji kufunguka pindi wakiziba na viroba jambo lililopelekea kamati ya umwagiliaji kutoza gunia mbili ili kukabiliana na changamoto hiyo.