Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia ofisi za Serikali kuchukua maeneo wanayoyatamani kwa manufaa yao binafsi badala ya kufuata taratibu za kununua maeneo hayo kihalali.
Pia, amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia haki za Watanzania bila kupepesa macho na kwamba wale wote wanaojifanya wababe dhidi ya haki za wananchi watachukuliwa hatua kali.
Aidha amesema kuwa ili nchi ipate maendeleo ni lazima kila mtu atimize wajibu wake huku haki za wananchi zikilindwa bila upendeleo.
Pia amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza wazi kuwa pamoja na Serikali kuhitaji uwekezaji na miradi ya maendeleo, viongozi hawapaswi kupora maeneo ya wananchi bila kuwalipa fidia yenye thamani halisi.
Ameyasema hayo Mei 08, 2026 wakati akizungumza na wakazi wa Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ambapo amesema kuwa Serikali inaendelea kupita katika maeneo mbalimbali kusikiliza kero za wananchi kama alivyoelekeza Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia amebainisha kuwa kuna baadhi ya watu wanaokwazika kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali, lakini ni lazima hatua hizo zichukuliwe ili kuhakikisha haki za Watanzania zinalindwa.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kushughulikia changamoto zote zinazowanyima wananchi furaha na haki zao ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata tabasamu.
Aidha amebainisha kuwa kumekuwa na tabia ya kupuuzapuuzwa kwa haki za wananchi pamoja na kukanyagwa na kunyang’anywa haki zao jambo alilolitaja kuwa ni mazoea mabaya yasiyokubalika.Pia amesema kuwa hatawavumilia watu wote wanaojihusisha na vitendo vya aina hiyo kwani kwa baadhi ya wananchi ardhi ndiyo mali yao pekee ukiondoa uhai wao.
Huku akibainisha kuwa sheria ziko wazi kuhusu masuala ya ardhi na zinaeleza wazi kuwa pale ardhi inapochukuliwa kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa, mwenye eneo anatakiwa kufidiwa kabla ya eneo hilo kuchukuliwa.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikirahisisha mno utaratibu huo kwa kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo bila kuwafidia wananchi husika.
ameongeza kuwa ni muhimu wananchi wanaochukuliwa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa shule, vituo vya afya au miradi mingine walipwe fidia ili waweze kupata maeneo mengine ya kuendelea na maisha yao.
