Na Jeremia Mwakyoma na Jeremiah Mbwambo, BMH
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA – MEI 8, 2026
MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz, amesema ameshangazwa na ukubwa pamoja na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH).
Amesema hakuwahi kujua kuwa jijini Dodoma kuna hospitali yenye uwezo mkubwa kiasi hicho ambayo inatoa huduma za kibingwa zipatazo 20 na ubingwa bobezi zaidi ya 17.
Diamond amesema hayo alipotembelea hospitali hiyo kujionea utoaji huduma ambapo alipata fursa ya kutembelea maabara maalumu ya uchunguzi na upasuaji wa moyo na mishipa ya damu (Cath. Lab), Kitengo maalumu cha upandikizaji Uloto, Kituo cha upandikizaji Figo na huduma nyingine za kibingwa hospitalini hapo, ambako alipata pia fursa ya kuzungumza na madaktari pamoja na wagonjwa waliokuwa wanapatiwa matibabu.
Amesema kazi inayofanywa na madaktari na wataalamu wa afya katika hospitali hiyo ni kubwa na yenye kugusa maisha ya Watanzania wengi.
“Nawapongeza madaktari wa BMH kwa kazi kubwa mnayofanya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu. Kazi yenu ya kuwahudumia na kuwafariji wagonjwa ni ya kipekee,” amesema Diamond.
Aidha, amewataka madaktari kuendelea kuwa wavumilivu kwa wagonjwa wanaowahudumia kila siku kutokana na changamoto mbalimbali wanazopitia.
Msanii huyo pia aliipongeza serikali pamoja na Wizara ya Afya kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya afya, akisema maendeleo ya BMH yanaonyesha dhamira ya serikali ya kuboresha huduma za matibabu nchini.
Alisema kutokana na huduma zinazotolewa hospitalini hapo, yupo tayari kuwa balozi wa kuitangaza BMH ili wananchi wengi zaidi wafahamu kuhusu huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazopatikana nchini.
“Kwa kweli sikutegemea kukuta hospitali kubwa na yenye huduma za kisasa kama hizi hapa Dodoma. Mitambo ya kisasa, huu ni uwekezaji mkubwa ambao unapaswa kuungwa mkono, Hospitali safi mazingira mazuri, haitoi harufu ya dawa,” amesema Diamond.
Alisema yeye pamoja na wasanii wenzake watakuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii na wadau mbalimbali kuiunga mkono hospitali hiyo ili iendelee kuboresha huduma zake.
Katika hatua nyingine, wasanii hao walitangaza michango mbalimbali kwa ajili ya kusaidia maboresho ya hospitali hiyo, ambapo yeye na watu walioambatana wameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 185.
Diamond amesisitiza kuwa huo ni mwanzo wa jitihada zao za kushirikiana na serikali katika kuimarisha huduma za afya na kuhakikisha hospitali hiyo inafikia malengo yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
