NA: MWANDISHI WETU, PANGANI.
Utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu unaozingatia umahiri kwa wanafunzi unaendelea kutekelezwa nchi nzima katika kuhakikisha nchi inazalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.
Katika Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga, Mei 8, 2026, wanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo, katika somo la Biashara (Business Studies), wameweza kupika vitafunwa mbalimbali kama chapati, maandazi, sambusa na vitumbua ikiwa ni sehemu ya ujifunzaji kwa vitendo wa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zilizo katika mazingira yao (local production).
Mwalimu wa somo la Biashara wa shule hiyo, Shija Clement amesema baada ya ujifunzaji wa nadharia wa Mada ya Uzalishaji (Production), wanafunzi wanapaswa kuweka ujifunzaji huo kwa vitendo ili kuwajenga katika umahiri na kujitegemea hata baada ya kuhitimu masomo yao ili pia waweze kujiajiri wenyewe na kuanzisha biashara zao.
“Wanafunzi wanapaswa kuwa na ujuzi fulani wanapohitimu masomo, wanafunzi hawa wamefanya kwa vitendo utengenezaji wa sambusa, chapati, maandazi na vitumbua lakini pia wamewauzia wanafunzi wenzao ili kuangalia kama uzalishaji wao umewapatia faida au hasara,” amesema Shija.
Sambamba na hilo, Shija amesema somo la Biashara linahitaji kufanya vitendo zaidi kwa sababu elimu ya biashara inapaswa kuwekwa katika vitendo ili tija ya kupata faida ionekane badala ya kubaki na maarifa ya biashara kichwani pekee.
Katika hatua nyingine, mwanafunzi ambaye ameshiriki kupika vitafunwa hivyo, Fatuma Madaba amesema amefurahia mapishi na ameongeza uelewa wa namna ya kupika vitafunwa hivyo, ujuzi ambao anaweza kutumia hata akimaliza shule katika kujiingizia kipato.
“Nimeongeza kitu kikubwa katika mapishi ya leo, elimu hii ya ujasiriamali tunayofundishwa imenisaidia kunijenga hata baada ya kuhitimu masomo yangu naweza kuingiza kipato,” amesema Madaba.
Kwa upande wa Mkuu wa Shule hiyo, Nassoro Gamba, amepongeza ubunifu huo ambao umejikita kuimarisha stadi za umahiri katika ujenzi wa vizazi vyenye kujitegemea katika maisha. Pia, ameahidi kuwa mteja wa kudumu wa bidhaa zao watakazoendelea kuzizalisha shuleni hapo.
Ikumbukwe kuwa somo la Biashara ni miongoni mwa masomo ya lazima kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini, ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi fulani katika kujipatia kipato ili kuepuka kusubiri kuajiriwa.

