Na.Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa ametoa maelekezo kwa watendaji wa sekta ya afya kuacha kuagiza dawa kutoka nje ya nchi na badala yake kutumia viwanda vya ndani vinavyozalisha dawa kwa viwango vya ubora, akisisitiza kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali.
Hayo ameyasema Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendeshaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba Mloganzila Mchengerwa alisema serikali haitavumilia udalali wa dawa unaochangia kupanda kwa gharama za tiba huku wazalishaji wa ndani wakikosa soko, akieleza kuwa Tanzania lazima ifikie lengo la kuongeza uzalishaji wa dawa kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 80 katika miaka ijayo.
Alisema mfumo wa “cluster” za viwanda vya dawa ni suluhisho muhimu litakalopunguza gharama za uwekezaji, kuharakisha uzalishaji na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani kwa kutumia miundombinu ya pamoja kama umeme, maji, mifumo ya usalama na maabara za ubora.
Aidha waziri Mchengerwa amesema, mfumo huo utawezesha pia usimamizi bora wa viwango vya kimataifa vya dawa, kuongeza uwekezaji mkubwa na kuimarisha uwezo wa taifa katika uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba.
Mchengerwa pia aliipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kutoa eneo la ardhi kwa ajili ya maendeleo ya cluster hiyo, akisema hatua hiyo ni ya kizalendo na ya kimkakati kwa mustakabali wa taifa.
Aidha, alisema serikali inataka cluster hiyo iwe kiungo kati ya elimu, utafiti na viwanda ili wanafunzi, watafiti na maprofesa washiriki moja kwa moja katika kutatua changamoto za uzalishaji wa dawa na teknolojia ya afya nchini.
Katika hatua nyingine, waziri huyo alitangaza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya imesaini makubaliano ya ushirikiano na kampuni kubwa ya kimataifa ya teknolojia ya chanjo kwa lengo la kujenga uwezo wa Tanzania katika uzalishaji wa chanjo za kisasa na teknolojia za afya.
Alisema ushirikiano huo utaisaidia Tanzania kupata maarifa, teknolojia na mifumo ya kisasa ya uzalishaji wa chanjo na dawa za kibayolojia, huku ukiiweka nchi katika nafasi ya kuwa kitovu cha teknolojia ya afya barani Afrika.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Emmanuel Tayari alisema serikali imeanza kutekeleza mkakati wa kitaifa wa cluster za viwanda vya dawa ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuvutia wawekezaji na kuimarisha usalama wa upatikanaji wa dawa nchini.
Alisema maeneo ya mwanzo yaliyopangwa kwa utekelezaji wa cluster hizo ni Mloganzila na Kibaha, huku maeneo mengine yaliyotengwa kwa maendeleo ya baadaye yakihusisha Bagamoyo, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara.
Alisema serikali kupitia TISEZA pia imepata ekari 1,000 Bagamoyo kwa ajili ya kuendeleza eneo maalumu la uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba, akibainisha kuwa lengo ni kujenga mfumo wa kisasa wa uzalishaji utakaoifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vya afya katika ukanda wa Afrika Mashariki.

