Baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseh Kashushura wa pili kulia na mwenyekiti wa Halmashauri Desderius Haule wa pili kushoto,wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kikao cha baraza la madiwan

………..

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

HALMASHAURI ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka lengo la  awali la Sh.bilioni 10 na kufikia Sh.bilioni 12.1 sawa na ongezeko la Sh.bilioni 2.1.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Joseph Kashushura amsema hayo jana,wakati akitoa taarifa ya mapato kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kujadili taarifa za robo ya tatu  kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Aidha alisema,Halmashauri hiyo inakusudia kukusanya zaidi ya Sh.milioni 200 kutoka kwenye jengo la uwekezaji la Mbinga Dc Mall lililopo Mbinga mjini ambapo katika kipindi cha miezi mitano  ya uendeshaji wa jengo hilo wamekusanya Sh.milioni 77.2.

Alisema, fedha zimetokana na michezo ya watoto Sh.milioni 11,kodi za wapangaji wa nyumba vya biashara Sh.milioni 43 na ukumbi kwa ajili ya shughuli na shughuli mbalimbali za wadau zimekusanywa Sh.milioni 22.

Kwa mujibu wa Kashushura,mradi wa uwekezaji wa Mbinga Mall pamoja na kuipa Halmashauri mapato umesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi wa mji wa Mbinga kama huduma za chakula,mavazi,vinywaji  na burudani mbalimbali.

Akizungumzia mapato yanatokanayo na makaa ya mawe alisema,makusanyo ya yamepungua kwa kiasi fulani ndiyo maana Halmashauri hiyo imejikita kwenye uwekezaji wa maeneo mengine ikiwemo Mbinga Mall ili kuendelea kuwa na vyanzo vingi zaidi vya mapato.

Mwakilishi wa katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Amandus Chilumba,ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma na kitaifa imeshika nafasi ya tatu.

Chilumba alisema,Serikali imepeleka jumla ya watumishi 250 wa kada mbalimbali ili kufanya kazi katika Halmashauri hiyo ambapo ameitaka Halmashauri kupitia madiwani kuishi vizuri na watumishi hao ili wasikifikirie kuondoka au kuacha kazi.

“Madiwani kaeni vizuri na watumishi wapya walioletwa katika maeneo yenu na mfahamu changamoto zao ili Serikali iweze kuchukua hatua na kuwasaidia,hawa ni vijana wenu wanahitaji msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku”alisema Chilumba.

Naye kuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori,amelipongeza baraza la madiwani na menejimenti ya Halmashauri hiyo kwa kuendelea kudumisha ushirikiano na kufanya kazi kwa weledi jambo linalochochea kasi kubwa ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.

“Nawapongeza namna mnavyofanya kazi kwa umoja,nawasihi sana endeleeni kulinda sifa na heshima ya Mbinga Dc na muwe makini na watu wanaowaonea wivukutokana na mafanikio yenu ili kuvunja umoja huu”alisema Makori.

Katika hatua nyingine,Makori amaewataka wataalamu kuweka  mpango madhubuti wa kuipandisha hadhi shule ya sekondari ya Mashujaa Litembo ili iwe shule ya kidato cha tano na sita(High School)ili kupanua wigo wa elimu kwa watoto na kupunguza umbali kwa kwenda nje ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya elimu ya juu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbinga Desderius Haule,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya kuleta maendeleo na kuboresha ustawi wa wananchi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga.

Haule,amewasisitiza madiwani kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata kutatua changamoto za wananchi badala ya kuwa watazamaji.