Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa ufafanuzi kuhusu sakata la wafanyabiashara wa lililokuwa soko la Rehema Nchimbi baada ya eneo hilo kufungwa, ikibainisha kuwa ilichukua hatua mbalimbali kuwapatia maeneo mbadala ya kuendelea na shughuli zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 4,2026 Jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, amesema kuwa Halmashauri ilipokea taarifa ya kufungwa kwa soko hilo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma baada ya malalamiko ya wafanyabiashara kukosa maeneo ya kufanyia biashara.
Amesema kuwa Halmashauri ilipendekeza masoko mbadala yakiwemo Job Ndugai, Tambukareli, Makole na Kikuyu Kusini, ambayo yalikuwa na uwezo wa kuwachukua wafanyabiashara hao takribani 297, lakini wakayakataa wakidai hayakuwa mwafaka kwa shughuli zao.
Aidha amebainisha kuwa kutokana na changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya aliunda kamati shirikishi ya wadau kutoka serikali na wafanyabiashara kwa lengo la kutafuta suluhisho la pamoja.
Ameongeza kuwa baada ya mchakato huo, kamati ilipendekeza wafanyabiashara hao kuhamia eneo la Umonga lililopo mtaa wa Kitenge, kata ya Majengo, ambalo lina ukubwa wa mita za mraba 8,621 na ni eneo la kimkakati kibiashara.
Amesema kuwa Halmashauri iliandaa mpango wa awamu mbili wa uendelezaji wa eneo hilo, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa vibanda vya muda kwa wafanyabiashara, huku miundombinu ya kisasa ikiendelea kujengwa hatua kwa hatua.
Aidha amebainisha kuwa tayari huduma muhimu kama choo cha kisasa na usawazishaji wa eneo zimekamilika ili kuwezesha shughuli za biashara kuanza.
Ameongeza kuwa kila mfanyabiashara atapatiwa eneo moja lenye ukubwa wa mita tatu kwa tatu kwa ajili ya kujenga kibanda cha muda, kwa kuzingatia orodha iliyohakikiwa na kamati husika.
Aidha amesema kuwa kikao cha kupitia rasimu ya mikataba kilifanyika Aprili 27, 2026, lakini wafanyabiashara walikataa kujadili agenda hiyo na badala yake kuibua hoja mpya ikiwemo ongezeko la wafanyabiashara na madai ya fidia.
Pia, amebainisha kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote aliyepewa au kuuziwa eneo kihalali katika eneo la Umonga, hivyo yeyote anayelipia eneo kabla ya utaratibu kukamilika anakuwa ametapeliwa.
Pia, ameongeza kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia mchakato huo hadi kukamilika kwa ugawaji rasmi wa maeneo kwa uwazi na ushirikishwaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Jiji la Dodoma, Bw. Nsubi Kapula amesema kama viongozi wa wafanyabiashara hawatashiriki kupitia rasimu ya mkataba, halmashauri itakutana moja kwa moja na wafanyabiashara kuhakikisha shughuli zinaanza kutekelezwa.
