Dodoma, Mei 02, 2026
Mkoa wa Dodoma umefikia hatua muhimu katika safari ya kujenga jamii salama, jumuishi na yenye haki kwa wote, kwa kuzindua rasmi Mpango Mkakati wa Mkoa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2026/27 hadi 2029/30. Uzinduzi huu umefanyika Mei 02,2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Jengo la Mkapa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, akiwa Mgeni Rasmi.
Mpango kazi huu ni zao la utambuzi wa kina wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayoendelea katika Mkoa wa Dodoma, sambamba na dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha kuwa ukuaji wa mkoa unaendana na ulinzi wa haki za msingi za binadamu, hususan wanawake na watoto ambao kwa muda mrefu wamekuwa waathirika wakuu wa vitendo vya kikatili .
Katika hotuba yake, Mhe. Senyamule alisisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea mshikamano wa wadau wote, Serikali, Sekta Binafsi, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla, akibainisha kuwa mapambano dhidi ya ukatili hayawezi kufanikiwa kwa juhudi za upande mmoja pekee. Alieleza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kupitia sera, sheria na mifumo ya utoaji haki, ikiwa ni pamoja na juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ameendelea kuonesha uongozi thabiti katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Alitoa pongezi mahsusi kwa uanzishwaji wa huduma ya Samia Legal Aid, ambayo imeongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi, hususan wanawake na watoto wasiokuwa na uelewa wa kutosha wa sheria. Alisisitiza kuwa ukosefu wa maarifa ya kisheria umekuwa kichocheo kikubwa cha ukatili, hivyo huduma hiyo ni nyenzo muhimu ya kuwezesha jamii kujitetea na kudai haki zao.
Aidha, alitambua mchango mkubwa wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum chini ya uongozi wa Dorothy Gwajima, kwa kuendelea kutoa miongozo, sera na mikakati inayowawezesha wadau wa mikoa kutekeleza kwa ufanisi ajenda ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Katika muktadha wa ukuaji wa kasi wa Jiji la Dodoma, uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na uhamiaji wa watumishi wa Umma na shughuli za kiuchumi zinazoongezeka, Mhe.
Senyamule alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, kuna changamoto mpya zinazohitaji hatua madhubuti. Maeneo ya Umma kama masoko, vituo vya usafiri na sehemu za burudani yameonekana kuwa vitovu vya matukio ya ukatili wa kijinsia, jambo linalohitaji mikakati mahsusi ya kinga, ulinzi na uelimishaji wa jamii.
Mpango kazi huo wa miaka minne umejikita katika nguzo kuu kadhaa ikiwemo:
kuimarisha mifumo ya kinga na utoaji huduma kwa waathirika, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki na sheria, kuimarisha uratibu wa wadau, pamoja na kutumia takwimu na ushahidi katika kupanga na kutekeleza afua. Vilevile, mpango huo unasisitiza uwajibikaji wa taasisi zote katika kuhakikisha kuwa hakuna mwanamke wala mtoto anayebaki nyuma katika kupata haki na ulinzi.
Mkoa wa Dodoma unaendelea kuchukua nafasi yake kama kitovu cha utawala wa Nchi, huku ukihakikisha kuwa maendeleo yake yanakuwa na sura ya utu, usawa na heshima kwa wote. Huu ndio mwelekeo, na huu ndio wajibu wa kizazi cha sasa.
