Picha no 634 Meneja wa huduma za maabara Hospitali ya misheni Litembo wilayani Mbinga Deograsias Ndunguru,akionyesha baadhi ya vifaa vya kuhifadhi damu na kutambu magonjwa mbalimbali kwa wagonjwa wanaofika katika Hospitali hiyo.
Picha no 648 Meneja wa huduma za maabara Hospitali ya misheni Litembo Deograsias Ndunguru,akionyesha namna wanavyohifadhi damu salama.
………..
Na Mwandishi maalum, Litembo-Mbinga
WATANZANIA wametakiwa kuwa wajasiri na moyo wa huruma kwa kuchangia damu mara kwa mara ili kuokoa maisha ya watu wengine hususani mama wajawazito,watoto njiti na wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu wanaofikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Wito huo umetolewa na meneja wa kitengo cha maabara katika Hospitali ya misheni Litembo iliyopo Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Deograsias Ndunguru.
Ndunguru alisema,damu ni hitaji la msingi katika huduma za dharura,upasuaji,uzazi na wagonjwa wenye maradhi kama vile kisukari,saratani,na watoto wenye upungufu wa damu.
Ndunguru alisema,kila tone la damu linaweza kuleta tofauti kati ya maisha ya mwanadamu na kifo,hivyo jamii inatakiwa kuwa na mazoea/utaratibu kwenda Hospitali ili kujitolea damu kwani hatua hiyo itasaidia kuziba pengo kubwa la upatikanaji wa damu salama hapa nchini.
“Uchangiaji damu ni wastani kwani licha ya taasisi yetu kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kupitia kampeni mbalimbali tunazofanya, lakini bado mwitiko ni mdogo”alisema Ndunguru.
Ndunguru alisema,mahitaji ya damu katika Hospitali ya Litembo kwa mwaka kwa wastani ni chupa 430 lakini zinazopatikana ni robo tatu ya mahitaji hivyo inapotokea mahitaji makubwa wanalazimika kuomba kwenye vituo vingine rafiki ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga,Hospitali ya wilaya Nyasa,kituo cha afya Kigonsera na Mapera.
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Litembo Evodia Komba,amewaomba wananchi wa maeneo ya jirani na wanaotoka nje ya kata ya Litembo wanaofika katika Hospitali hiyo kwa ajili ya kupata matibabu waone umuhimu wa kuchangia damu kwa ajili ya ndugu na jamii wanaohitaji kuongezewa damu ili kuokoa maisha yao.
“Suala la damu ni muhimu sana kwa maisha yetu sisi binadamu,huku Mbinga ajali za boda boda ni nyingi kutokana na jiografia ya wilaya yetu ambayo ni milima na mabonde na matukio ya ajali ni mengi na majeruhi wanaoletwa katika Hospitali hii wanaohitaji kuongezewa damu ni wengi,tunawaomba sana watu wanaokuja kupata huduma mbalimbali wajitokeze kuchangia damu”alisema Komba.
Takwimu kutoka wizara ya afya zinaonyesha kuwa,mahitaji ya damu salama hapa nchini ni chupa 550,000 kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya afya huku mpango wa Taifa wa damu salama(NBTS) hukusanya wastani wa chupa 350,000 lakini kati ya hizo asilimia 15 huwa hazitumiki kutokana na changamoto kama uhifadhi usio salama au uchunguzi wa kiafya wa damu.