▪︎ Asema ujenzi uendelee hadi kukamilisha km 58 zote kwa kiwango cha lami

▪︎ Asisitiza kukamilishwa kwa usanifu na upatikanaji wa fedha kwa wakati

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mtili–Ifwagi–Mdabulo–Lulanda (km 58) kwa kiwango cha lami, huku akiagiza hatua za haraka zichukuliwe kukamilisha sehemu zilizosalia ili barabara hiyo iweze kutoa huduma kwa ukamilifu.

Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 2, 2026, alipotembelea na kukagua mradi huo katika Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, ambapo alipokea taarifa ya utekelezaji na kujionea maendeleo ya ujenzi uliofikia hatua mbalimbali.

“Nimeambiwa tayari kilomita kumi na nne zimeshajengwa na nimeona… tutaendelea kujenga barabara hii kwa sababu bado kuna kilomita zingine, ili iweze kutoa huduma kwa ukamilifu wake,” amesema.

Mradi huo unatekelezwa kupitia mpango wa Roads to Inclusion and Socio-Economic Opportunities (RISE) unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia, ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu ya barabara vijijini, kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, hadi sasa ujenzi wa kipande cha Mtili–Ifwagi (km 14) umekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 21, huku mradi mzima ukiwa umefikia takriban asilimia 57 ya utekelezaji katika awamu mbalimbali.

Akizungumzia hatua zinazofuata, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuharakisha usanifu wa sehemu zilizosalia ili kuuwezesha mradi kuingizwa kwenye bajeti na kuanza ujenzi wake kwa wakati.

“Ikamilisheni haraka usanifu… mpaka tunapomaliza mwezi wa sita tujue mmefikia hatua gani ili tuweze kusukuma masuala ya fedha na utekelezaji wake uanze mara moja,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa barabara hiyo ni ya kimkakati kwa uchumi wa eneo hilo kutokana na mchango wake katika usafirishaji wa mazao ya misitu, chai na mazao mengine ya kilimo.

“Barabara hii ni barabara muhimu, ni barabara ya kiuchumi… magari yanabeba mbao na mazao ya viwandani, wakati mwingine yanakwama, sasa ni wakati wa kuijenga barabara hiyo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wataalamu na wasimamizi wa mradi huo kufanya kazi kwa kasi na ubunifu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.

“Ni barabara za uzalishaji… ikimbizeni hata kama mtafanya kazi usiku na mchana,” amesema.

Waziri Mkuu pia amewapongeza TARURA na wadau wa mradi kwa utekelezaji mzuri wa kipande kilichokamilika, hususan kwa kuzingatia usalama wa watumiaji wa barabara wakiwemo watembea kwa miguu.

Awali, taarifa ya mradi ilieleza kuwa kukamilika kwa kipande hicho cha barabara kumeongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, pamoja na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Mufindi na maeneo jirani.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara ili kuchochea maendeleo ya uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.