Wahandisi watatu wa rasilimali za maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika (LTBWB) mkoani Kigoma wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma wakikabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi na ubadhirifu wa fedha kiasi cha Shilingi milioni 103.

Kesi hiyo namba ECC.9258/2026 imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Mhe. Anna Kuhungu, ambapo washitakiwa hao ni Kulwa Ryoba James, Gaudens John Ndolo na Pamhilius Gerald Gagwa.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili kutoka TAKUKURU, Bw. Augustino Lohay na James Nyarobi, uliieleza mahakama kuwa washitakiwa wanakabiliwa na makosa ya matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri, ufujaji na ubadhirifu, kusaidia kutendeka kwa kosa pamoja na kughushi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 22, 28(1) na 30 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 R.E 2022, vikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 Marejeo ya mwaka 2022, pamoja na vifungu vya 333, 335(a) na 335(b)(i)(ii) vya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.

Inadaiwa kuwa kati ya mwezi Julai na Agosti 2022, washitakiwa walitenda makosa hayo kwa kutumia hati za malipo zenye thamani ya Shilingi 103,000,000 mali ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika Kigoma Mjini, zikiwa na maelezo ya uongo ya kuwalipa watumishi hewa wakati wa zoezi la kutambua na kukagua vyanzo vya maji katika wilaya za Kibondo, Kakonko, Biharamulo na Ngara.

Washitakiwa wote wamekana mashtaka yanayowakabili mahakamani hapo.

Aidha, washitakiwa wamepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama.

Shauri hilo limeahirishwa na linatarajiwa kuendelea kusikilizwa tena Mei 14, 2026.