Na Atley Kuni, WAF-Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Afya wameshekea Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kwa kufanya matendo ya Huruma mara baada ya kuchangia vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi Mil. 15 kwa wahitaji katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.

Zoezi hilo limefanyika Leo Mei Mosi, 2026 katika Viunga vya Hospitali hiyo jijini Dodoma mara baaada ya kushiriki, Maandamano ya Wafanyakazi, kusikiliza Hotuba za Viongozi kisha kwenda Hospitalini hapo kwa ajili ya kukamilisha matendo hayo ya huruma. 

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vitu hivyo, Mratibu wa zoezi Bi. Tumaini Didier ambaye ni Afisa Utumishi Mwandamizi kwa niaba ya watumishi wa Wizara ya Afya, amesema wamewiwa kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kukumbuka wahitaji ambao kwa namna moja au nyingine hawana uwezo huo.

“Hii ni nguvu kazi, lakini kutokana na kuwa na matatizo ya afya ya akili, hata uwezo wa uzalishaji umeathirika siyo kama walipenda kuwa katika hali hiyo hivyo, kwa watumishi kuja hapa kwa ajili ya kuwapa misaada ni kutambua uhitaji wao”, amesema Bi. Tumain.

Akishukuru kwa niaba ya jamii ya wanamirembe, Pasnai Kivuyo, Afisa Ubora na Mwenyekiti wa misaada inayopelekwa kwa wagonjwa, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutambua uhitaji wao.

“Wagonjwa tulionao hapa, wanahudumiwa na Serikali kwa asilimia 100, hakuna ndugu wanaoshiriki isipokuwa baadhi ya watu mmoja mmoja, kwa mantiki hiyo basi tunapo pokea misaaada kama hii inatupunguzia gharama walau kidogo ya kuwahudumia jamii hii tunayoishi nayo”, amesema Bi. Kivuyo.

Vitu vilivyo kabidhiwa ni pamoja na Mchele, Mafuta ya kupikia, Sabuni za Kufulia, Kuogea na kufanyia usafi, Unga wa Ugali pamoja na Sukari, ambavyo vyote vinathamani ya Mil. 15.