Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amewataka waajiri nchini kuzingatia maslahi ya wafanyakazi wao ili kuhakikisha kunakuwa na ustawi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza leo, Mei 1, 2026, katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mhe. Chalamila, amesema kuwa amesisitiza kuwa wafanyakazi wanapopewa haki, stahiki pamoja na kuwa mazingira bora ya kazi, huchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Chalamila amesema kuwa wajibu wa waajiri ni kuhakikisha wanazingatia sheria za kazi pamoja na kutoa stahiki nyingine muhimu kwa wafanyakazi.

Aidha, Mhe. Chalamila amewataka wafanyakazi, hususan wa sekta binafsi na umma kuzingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na nidhamu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku. Huku akieleza kuwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kutachangia kuongeza tija, kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa taifa.

Katika maadhimisho hayo wafanyakazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wameungana na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, wakiahidi kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufikia malengo.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.” ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mhe. Albert Chalamila.