NA DENIS MLOWE IRINGA
MKUTANO wa Baraza la Madiwani Robo ya Tatu wa mwaka wa fedha 2025/2026 wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa umetamatika huku ukijikita katika kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza uwajibikaji katika ngazi zote za utendaji.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Wilaya ya Iringa DC, Steven Mhapa, amewasisitiza madiwani kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikamilifu katika kuisimamia miradi ya maendeleo kwenye kata zao.
 Ametaja kuwa usimamizi makini na ufuatiliaji wa karibu ndiyo msingi wa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma bora na miradi inakamilika kwa wakati.
Katika siku ya kwanza ya mkutano, Aprili 29, 2026, madiwani waliwasilisha taarifa za kata zao, wakieleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu, afya, miundombinu na huduma za kijamii.
Siku ya pili ya mkutano, Aprili 30, 2026, ilihusu kupitia kwa kina miradi ya maendeleo, ambapo wajumbe walijadili mapungufu yaliyobainika na kuweka mikakati ya kuyafanyia kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji.
Mwenyekiti Mhapa amesisitiza kuwa Baraza lina wajibu wa kuhakikisha rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo zinatumika ipasavyo, na akawataka madiwani kuendelea kushirikiana na watendaji pamoja na wananchi ili kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Iringa.