#Asisitiza umuhimu wa kulipa Kodi ya ardhi kwa wakati
#Aahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili
Na Munir Shemweta, KIGOMA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amekutana na kumfanya mazungumzo na wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Kigoma zikiwemo taasisi za umma na binafsi. Kiasi cha shilingi Bilioni 6.2 kinadaiwa kwa taasisi hizo na watu binafsi mkoani humo.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 30 April, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Mhe. Dkt Akwilapo amesema kati ya kiasi hicho cha fedha taasisi za umma pekee zinadaiwa shilingi Bilioni 5.8, taasisi binafsi milioni 272.4 na watu binafsi miliomi 116.4.
‘’Kila mtu anayemiliki kipande cha ardhi ana haki na wajibu wa kulipa kodi ya pango la ardhi Kwa mujibu wa Sheria ya ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999’’. Amesema Dkt Akwilapo
Amewaelekeza makamisha wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kuanza kuchukua hatua kwa wadaiwa ambao hawajatekeleza wajibu wao wa kisheria wa kulipa Kodi ya ardhi kwa kutii Sheria.
“Niwakumbushe wote wasiolipa kodi ya pango la ardhi hata kama hawajatumiwa ankara za Kodi wafike Ofisi za Ardhi za Mikoa ili waelezwe na kupewa ankara kuepuka malimbikizo ya madeni,riba pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wamiliki wa ardhi waliobadilisha Namba za simu kwenda Ofisi za Ardhi kuhuisha namba zao za simu ili waweze kupata Ankara za bili zao kupitia jumbe za simu za mkononi.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za sekta ya ardhi kwa haraka, Mhe. Dkt Akwilapo amewataka wananchi kufika katika Kliniki za ardhi zinazoendeshwa maeneo mbalimbali nchini ili waweze kuhudumiwa.
Awali taasisi za umma na binafsi kupitia wawakilishi wao walimueleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baadhi ya changamoto wanazopata wakati wa kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi ambapo wametaja moja ya changamoto hizo ni kukadiriwa kodi kwa eneo kubwa tofauti na uhalisia wa eneo husika wanalomiliki.
” Tunaenda kulipa kitu ambacho hatukitumii, eneo letu ni square mita 1,129 lakini wewe Ofisi unatuambiwa tunadaiwa square mita 5,000 ni haki kwelii? Amesema mmoja wa wadaiwa sugu.
Dkt Akwilapo aliziahidi taasisi hizo za umma, binafsi pamoja na wananchi wengine kuwa changamoto walizowasilsha kwake zitafanyiwa kazi ndani ya muda mchache na kuomba ushirikiano wakati wote wa kushughulikia changamoto hizo.

(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
