Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) wameungana na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika leo, Mei 1, 2026, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu wa ETDCO, Bw. Thomas Mwinuka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni hiyo, Bi. Veneranda Gervas kutoka Idara ya Manunuzi na Ugavi ambaye amechaguliwa kuwa Mfanyakazi Bora wa mwaka 2026 (kulia) na Bw. Erasto Matola kutoka Idara ya Ufundi aliyeshika nafasi ya pili wakiwa katika hafla ya kusherekea siku ya wafanyakazi Duniani

………

Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) wameungana na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, wakiahidi kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufikia malengo ya Kampuni.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo, Mei 1, 2026, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu wa ETDCO, Bw. Thomas Mwinuka, amesema kuwa uongozi wa Kampuni umejipanga kuweka mikakati rafiki inayolenga kuongeza hamasa kwa wafanyakazi, hususani katika kuimarisha ushirikiano kazini ili kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

“ETDCO itaendelea kuimarisha mazingira bora ya kazi na kuhamasisha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi, jambo ambalo litachochea ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya umeme nchini,” amesema Mwinuka.

Aidha, amewataka wafanyakazi kuongeza bidii na kuwajibika kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ya kila siku ili kusaidia kufikia lengo la kutoa huduma bora na ya uhakika ya umeme kwa wananchi.

Kwa upande wao, wafanyakazi wa Kampuni hiyo, akiwemo Bi. Veneranda Gervas kutoka Idara ya Manunuzi na Ugavi ambaye amechaguliwa kuwa Mfanyakazi Bora wa mwaka 2026, pamoja na Bw. Erasto Matola kutoka Idara ya Ufundi aliyeshika nafasi ya pili, wameushukuru uongozi wa kampuni kwa kuonesha ushirikiano kwa wafanyakazi na kuthamini utekelezaji wao wa majukumu.

“Leo tunajivunia mshikamano, ushirikiano na upendo tuliojengewa na uongozi wa ETDCO. Hii imetuwezesha kutekeleza miradi kwa wakati na kwa mafanikio makubwa,” amesema Gervas.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.” Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo katika mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Albert Chalamila.