Mkurugenzi wa Hospitali Litembo Padre Rapahael Ndunguru,akizungumzia ubovu wa barabara ya Mbinga-Litembo ambayo imekuwa kikwazo kikubwa wananchi hususani wagonjwa kushindwa kupata huduma kwa wakati kwani wanatumia muda mwingi barabarani kabla ya kufika.
…………….
Na Mwandishi Maalum, Litembo
UBOVU wa barabara ya Mbinga-Litembo Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoa wa Ruvuma inayosimamiwa na Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kuwa kilio kikubwa kwa wananchi wa kata ya Litembo na maeneo mengine ya wilaya hiyo kutokana na kuharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha.
Wananchi,wameiomba Serikali kutimiza ahadi ya kujenga barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 28 kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri wanapokwenda Hospitali ya Litembo ili kupata matibabu na wengine kusafirisa mazao hususani zao la kahawa.
Wamesema,barabara hiyo ni mbaya na baadhi ya wagonjwa wanashindwa kufika Hospitali ya Litembo iliyopo kijiji cha Litembo kupata matibabu kwa wakati kwa sababu wanatumia muda mwingi barabarani.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Litembo Padre Raphael Ndunguru alisema,katika kijiji cha Litembo kuna huduma nyingi za kijamii ikiwemo Hospitali,benki,chuo cha afya na shule mbili za sekondari.
Alisema,Hospitali ya Litembo imekuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka nje na ndani ya nchi hata kwa wanafunzi wanaofika kufanya mazoezi kwa vitendo.
“Changamoto kubwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara kutoka Mbinga mjini hadi kijiji cha Litembo kilometa 28 tu,lakini zimekuwa kero kubwa sana kwa watumiaji hasa akina mama wajawazito na wagonjwa wanaoletwa kutoka kwenye vituo mbalimbali kuja Hospitali ya Litembo kupata huduma zaidi”alisema Padre Ndunguru.
Padre Ndunguru alisema,endapo hatua za haraka hazitachukuliwa,hiyo itaendelea kuathiri ustawi wa wananchi na kudhoofisha juhudi za maendeleo katika kata ya Litembo na wilaya ya Mbinga kwa ujumla.
Alisema,kama Serikali itaifungua barabara hiyo na kujenga kwa kiwango lami, itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Litembo na tarafa nzima ya Mbuji.
Mkazi wa kijiji cha Litembo Elizabeth Komba alisema,mama wajawazito ndiyo waanga wakubwa na wapo wanaojifungua na kufariki dunia wakiwa njiani kabla ya kufika Hospitali kwa kuwa wanatumia muda mrefu kufika Hospitali.
Aisha Said mkazi wa kijiji cha Kitai alisema, barabara ya Mbinga-Litembo ni changamoto kubwa kutokana na ubovu wake,hali inayopelekea washindwe kufika Hospitali Litembo kwa wakatikwa ajili ya kupata huduma za afya na kufanya kazi nyingine za kiuchumi.
“Hii Hospitali ya Litembo ni mkombozi mkubwa kwetu sisi wananchi wa wilaya ya Mbinga kutokana na uwepo wa huduma bora hasa madaktari bingwa,lakini tatizo kubwa ni namna ya kufika kirahisi kutokana na ubovu wa barabara,tunaiomba sana Serikali yetu ijenge barabara hii kwa lami kwani tumechoka kuteseka”alisema Said.
Mkazi wa kijiji cha Kitula Antony Komba alisema kuwa,wakiacha hali hiyo iendelee wakulima wa kahawa watalazimika kuuza mazao kwa njia ya haramu ya magoma kwa walanguzi kwa sababu watashindwa kupeleka kwenye maghala ya chama kikuu(Mbifacu) Mbinga mjini.
Alisema,mvua zinazoendelea kunyesha zimezidisha ubovu wa barabara hiyo,hali inayosababisha baadhi ya maeneo kushindwa kupitika kirahisi na kuwaweka wananchi katika wakati mgumu wa usafiri na mawasiliano.
Alisema,changamoto ya barabara imeathiri sana shughuli za kiuchumi,hususani kwa wakulima wanaotegemea barabara hiyo kusafirisha mazao yao kwenda sokoni hali inayopunguza kipato chao na kudumaza maendeleo.
“Barabara hii imekuwa kama mradi kwa wagombea kwani unapofika muda wa uchaguzi wanakuja na wanatoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami,lakini baada ya kuchaguliwa hawaonekani tena,tunaiomba sana Serikali kupitia Tanroads mkoa wa Ruvuma iwe na huruma kwetu sisi wananchi wa vijijini”alisema.
Alipotafutwa meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma ili kutoa ufafanuzi wa changamoto hiyo hakupatikana kwani alikuwa nje ya ofisi na simu yake iliita bila kupokelewa,hata hivyo juhudi zinaendelea ili kujua mpango wa Serikali kupitia Tanroads kumaliza kilio cha wananchi hao zinaendelea.
