Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani), Aprili 30, 2026 wakati wa kutangaza kuanza kwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia awamu ya pili mkoani Dodoma 

Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, ametangaza kuanza kwa awamu ya pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama  Samia itakayoanza Mei Mosi hadi Mei 15, 2026, kwa lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi,huku  ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa huduma za kisheria bila malipo.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 30,2026 Jijini Dodoma, amesema kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi, hususan makundi yenye uhitaji, wanapata haki zao kwa urahisi.

Amesema kuwa makundi yatakayolengwa zaidi ni wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu pamoja na vijana, ambao mara nyingi hukumbana na changamoto ya upatikanaji wa huduma za kisheria.

Amebainisha kuwa Huduma za msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Mama Samia zitatolewa katika vituo mbalimbali vya Mkoa wa Dodoma. Katika Jiji la Dodoma huduma zitapatikana Uwanja wa Mtekelezo mkabala na Msikiti wa Gadafi, Chamwino (Buigiri na Mlowa Barabarani), Kongwa (Kibaigwa na Mkoka), Mpwapwa (Mpwapwa Mjini na Kibakwe), Bahi (Mwachubu Senta), Chemba (Kijiji cha Chemba), Kondoa Mjini (Stendi ya Zamani) na Wilaya ya Kondoa (Pahi Senta). Vituo hivyo vimewekwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi karibu na maeneo yao.

Aidha amebainisha kuwa utekelezaji wa awamu ya kwanza mwaka 2023 ulileta mafanikio makubwa ambapo jumla ya wananchi 86,947 walifikiwa na kupatiwa huduma hizo, wakiwemo wanaume 42,298 na wanawake 44,649.

Pia ameongeza kuwa kati ya migogoro 818 iliyopokelewa, jumla ya migogoro 452 ilitatuliwa huku mingine 366 ikiendelea kufanyiwa kazi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendeleza kampeni hiyo.

Amesema kuwa kampeni hiyo itaanza rasmi Mei Mosi hadi Mei 15, 2026 katika Mkoa wa Dodoma, ambapo wananchi watapatiwa huduma mbalimbali bila malipo ikiwemo ushauri wa kisheria, elimu ya sheria, uandaaji wa nyaraka, uwakilishi mahakamani na katika mabaraza, pamoja na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.

Aidha amebainisha kuwa huduma za usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo zitatolewa kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kurahisisha upatikanaji wa nyaraka muhimu kwa wananchi.

Pia ameongeza kuwa elimu kwa umma itatolewa katika ngazi mbalimbali kuanzia wilaya, kata hadi mitaa na vijiji, sambamba na kufanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama masoko, vituo vya mabasi, taasisi za elimu na mikusanyiko ya kijamii.Aidha, amebainisha kvituo vya huduma vitawekwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma kwa ukaribu zaidi.

Pia, ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo muhimu, akisisitiza kuwa upatikanaji wa haki ni haki ya msingi ya kila binadamu.

Kampeni hiyo inaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 yanayolenga kujenga jamii yenye usawa na ustawi kwa wote.