Na Jeremia Mwakyoma na Jeremiah Mbwambo,BMH
DODOMA – APRILI 29, 2026
Imeelezwa kuwa tatizo la usugu wa vimelea vinavyosababisha magonjwa dhidi ya dawa za kupambana na vimelea hivyo linazidi kuongezeka katika jamii.
Wataalamu wa Afya wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamebainisha hayo leo hii wakati wa kikao cha mafunzo ya Afya.
Mkurugenzi wa Huduma Shirikishi wa BMH Dkt. Abdallah Baja amesema kuwa vimelea na wadudu wa kusababisha magonjwa wanajitengenezea nguvu, uwezo na ulinzi dhidi ya dawa hizo; dawa zinakuwa hazina nguvu tena ya kuweza kuwadhibiti wadudu hao na hiyo inazidisha madhara zaidi endapo mtu akiugua.
Akiwasilisha Mada katika kikao hicho Daktari Bingwa wa Watoto na Mwenyekiti wa Timu ya kufuatilia matumizi sahihi ya Dawa (BMH) Emmy Mbilinyi amesema kuwa Dawa hizo zinazotumika kuua wadudu wanaoambukiza magonjwa (Antimicrobial) zinajumuisha Dawa zinazoua Fangasi, Virusi, Bakteria mbalimbali na vimelea ambao wote wanasababisha magonjwa.
“Bado jamii haina uelewa wa kutosha wa tatizo hili la usugu wa Dawa mwilini, mambo yanayosababisha tatizo hili ni pamoja na matumizi holela ya dawa bila maelekezo ya Daktari na wataalamu wa Afya, Kutokukamilisha dozi, Matumizi ya Dawa kama za Antibiotic pasipo ushahidi wa uchunguzi wa kimaabara, (kujimezea dawa kiholela), matumizi ya mimea na nyama zenye vimelea vya dawa hizo na Wataalamu wa Afya kutozingatia miongozo ya matibabu na utoaji Dawa amesisitiza Dkt. Mbilinyi.
Meneja wa Maabara ya BMH Dkt. Farida Mbura amesisitiza kuwa ili kusaidia kupunguza tatizo hili, ni muhimu Madaktari na Wataalamu wa huduma za Afya wakafuata vizuri Muongozo wa Uchunguzi na Matibabu sahihi kwa Wagonjwa.
Daktari Bingwa wa Upasuaji Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu Mugisha Nkoronko amesisitiza wagonjwa wanaokuja kutibiwa BMH wapewe somo kuhusu tatizo hili, pia jamii kwa ujumla kupitia vyombo vya Habari ielimishwe juu ya matumizi sahihi ya dawa (right Diagnosis, right treatment, right time and right dose).

