Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita haitavumilia kuona mwananchi akishindwa kupata dawa au huduma za afya kutokana na gharama, akisisitiza kuwa suala hilo ni kipaumbele cha kitaifa.
Akizungumza na wananchi katika maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Zimbwini wilayani Kibiti, amesema serikali imejikita katika kuboresha huduma za chanjo, bima ya afya kwa wote pamoja na usafi wa mazingira.
Amesema dhamira hiyo inaongozwa na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa usawa na kwa wakati.
Mchengerwa amesema afya ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kuwa endelevu bila kuwepo kwa jamii yenye afya bora.
Amesema wizara yake imeendelea kuandaa mipango na bajeti kwa kuzingatia sera ya afya ya mwaka 2022 hadi 2025 pamoja na makubaliano ya kimataifa yanayolenga kuimarisha huduma za afya nchini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, amesema ajenda ya serikali inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kuimarisha kinga kabla ya tiba, kuboresha ubora wa huduma pamoja na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa utu na heshima.
Amesema serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi taifa ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekosa huduma kutokana na umbali au changamoto nyingine.
Aidha, amesema serikali inaendelea kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya na kwa sasa zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanapata huduma ndani ya umbali unaokubalika.
Mchengerwa amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, vituo vya afya zaidi ya 3,500 vimejengwa na kuongeza idadi ya vituo hivyo kutoka 10,153 mwaka 2021 hadi kufikia 13,683 kwa sasa.
Amesema hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hususan kwa akina mama wajawazito na watoto.
Katika kuboresha zaidi huduma, amesema kuna mpango wa ujenzi wa hospitali ya kisasa ya mkoa katika eneo la Nyamwage itakayohudumia wananchi wa Kibiti, Rufiji, Kilwa na maeneo jirani.
Amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutapunguza rufaa zisizo za lazima kwenda Dar es Salaam na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Mchengerwa amehitimisha kwa kusema watumishi wa afya wanapaswa kuendelea kutoa huduma kwa weledi, utu na heshima huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika wataalamu, vifaa tiba na miundombinu ili kufikia lengo la asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

