Maafisa Usafirishaji maarufu kwa jina la Bodaboda wa Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya wahimizwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe Josephine Manase Aprili 28, 2026 wakati akifungua mashindano ya Mpira wa Miguu ya “Kyela Polisi Jamii Bodaboda Super Cup, 2026 yaliyokuwa yakifanyika katika uwanja wa Polisi Kyela na kushirikisha Maafisa Usafirishaji wa Wilaya hiyo kutoka katika Kata 33.
Mhe Manase amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuilinda Amani iliyopo kwa kuacha na kujiepusha kujihusisha na makundi yasiyofaa, vitendo visivyofaa katika jamii na badala yake washirikiane na Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kufichua wahalifu.
Aidha, Mhe Manase amepongeza mikakati thabiti ya Jeshi la Polisi Wilayani humo katika kuzuia uhalifu kupitia utekelezaji wa falsafa ya Polisi Jamii ambayo imekuwa ikishirikisha wananchi, kuwajengea uwezo na uelewa wa masuala ya usalama hali inayopelekea kupata mafanikio katika kuzuia uhalifu.
Mkuu wa kitengo cha ushirikishwaji wa Jamii, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Henry Mwaibambe kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma amewasihi wananchi wa Kyela kuilinda Amani iliyopo na kuacha kusikiliza maneno yenye nia ya kuvuruga amani na utulivu uliopo kwani kwenye amani watakuwa huru kufanya kazi zao za uzalishaji mali.
Naye, Diwani wa Kata ya Mikoroshini Gwakisa Mwakipesile amesema kuwa mashindano hayo yamekuwa na faida kubwa kwa vijana hasa Bodaboda kwani yamerejesha imani kati ya Jeshi la Polisi na Wananchi wa Kyela ambapo ushirikiano huo ni ishara ya mahusiano mazuri katika kukabiliana na uhalifu.
Kwa upande wake, Joshua Mwaisumo, Mkazi wa Kyela amepongeza waandaaji wa mashindano hayo kwani yamesaidia kuisogeza jamii karibu na Jeshi la Polisi na kusaidia jamii kupata elimu, kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na hatimaye Kyela kuwa salama.
Fainali ya mashindano hayo yalizikutanisha timu za Bodaboda Kata ya Ipinda dhidi ya Bodaboda Kata ya Serengeti na kushuhudia Bodaboda Kata ya Ipinda kuibuka mabingwa kwa changamoto za penati 5 kwa 3 na kuzawadi Ng’ombe, Jezi na Mpira. Mashindano hayo yalibeba ujumbe unaosema, “Amani, Utulivu na Mshikamano, kwa usalama na Maendeleo yetu”





