Na Hellen Mtereko,Mwanza
Koplo Stella Lyimo, mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana, Mkoani Mwanza, amemkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza tuzo na vyeti alivyoipokea tarehe 25 Aprili 2026, katika hafla iliyofanyika leo, 29 Aprili 2026, katika Bwalo la Polisi Mabatini.
Akipokea tuzo na vyeti hivyo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, amesema kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuthamini na kutambua mchango wa kila askari anayefanya vizuri katika majukumu yake. Aidha, aliwataka askari wote kuongeza juhudi na nidhamu mahali pa kazi.
“Ninawataka askari wengine kuwajibika kikamilifu kwa kuwahudumia wananchi na kulinda raia pamoja na mali zao kama inavyopaswa.Tunalenga kuwa na taasisi inayoheshimika na kupendwa na wananchi,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Katika taarifa iliyosomwa mbele ya Kamanda Mutafungwa, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, SSP Virginia Sodoka, alibainisha kuwa Koplo Stella amekuwa akifanya kazi kwa umahiri mkubwa, jambo lililovutia wananchi na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali kushirikiana naye.
“Koplo Stella aling’ara katika kipengele cha Ustawi wa Jamii kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, hatua iliyoleta matokeo chanya,” aliongeza SSP Sodoka.
Baadhi ya wafanyakazi wenzake, wakiwemo Inspekta Ernest Kagege, SP Prischal Sarabanze, na Sajenti Rodric Ndyamukama, wamempongeza Koplo Stella kwa kazi yake iliyotukuka na kumtia moyo kuendeleza kasi hiyo ya utendaji.
Akizungumza baada ya kukabidhi tuzo, Koplo Stella, ambaye hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya ‘Mwanamke Kinara’ katika kipengele cha Ustawi wa Jamii, amelishukuru Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla kwa ushirikiano waliompatia. Alieleza kuwa ushirikiano huo ulimwezesha kufikisha elimu kwa ufanisi, hali iliyopelekea wananchi wengi kubadilika na kuacha vitendo vya ukatili.
“Tuzo hii ni chachu kwangu ya kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na weledi wa hali ya juu, ili kuhakikisha jamii inazidi kuliamini Jeshi la Polisi na kuendelea kushirikiana nasi katika masuala mbalimbali ya kijamii,” alihitimisha Koplo Stella.
Koplo Stella Lyimo aliyechukua tuzo ya mwanamke kinara akizungumza




