Na John Bukuku, Kibiti
Serikali kupitia ushirikiano na wadau wa afya, ikiwemo Gavi, imekabidhi boti saba zenye thamani ya Sh1.1 bilioni kwa ajili ya kuimarisha huduma za chanjo katika maeneo ya visiwa na mwambao wa Bahari ya Hindi, hatua inayolenga kuwafikia wananchi waliokuwa wakikosa huduma kutokana na changamoto za kijiografia.
Akizungumza leo Aprili 29, 2026 katika Bandari ya Nyamisati wilayani Kibiti mkoani Pwani wakati wa makabidhiano ya boti hizo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesisitiza matumizi sahihi ya vitendea kazi hivyo, akitaka nidhamu, uwajibikaji na uzingatiaji wa taratibu za usalama viwe kipaumbele.
“Ni muhimu kuhakikisha boti hizi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Kila safari izingatie usalama, ikiwemo kutobeba zaidi ya abiria wanane na kufuata ratiba rasmi za huduma za chanjo,” amesema.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za afya hazibaki kuwa za hiari, bali zinawafikia Watanzania wote kwa ubora na kwa wakati, bila kujali changamoto za miundombinu au jiografia.
Mchengerwa amesema boti hizo zitasaidia kutekeleza majukumu makuu manne, ikiwemo kupanua wigo wa kuwafikia walengwa, kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa uhakika, kuimarisha usimamizi shirikishi wa huduma za afya na kuongeza uwezo wa utoaji huduma tembezi kwa wakati.
Ameeleza kuwa maeneo ya mwambao na visiwa yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya miundombinu, hali inayosababisha baadhi ya watoto kukosa chanjo kwa wakati na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa yanayozuilika.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Grace Magembe, amesema boti hizo zitasaidia kufikia watoto ambao hawajapata hata dozi moja ya chanjo (zero dose), ambao wengi wao wanapatikana katika maeneo ya mwambao na yasiyofikika kirahisi.
“Boti hizi zitaenda katika maeneo yenye changamoto kama Kibiti, Rufiji, Kigoma, Uvinza na Zanzibar. Lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma,” amesema.
Aidha, amesema pamoja na utoaji wa chanjo, boti hizo pia zitatumika kutoa huduma nyingine za afya ikiwemo elimu ya lishe na huduma mkoba kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mwakilishi Mkazi wa UNICEF nchini, Elke Wisch, ameipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika chanjo, akisema nchi imeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto.
“Tunapoadhimisha Wiki ya Afya, ni lazima tuhakikishe kila mtoto anayezaliwa Tanzania anapata chanjo zote muhimu za kuokoa maisha. Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa amemwagiza Mary Nagu kuhakikisha kituo cha afya Kibiti kinaboreshwa, huku akiagiza kutengwa kwa Sh 500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kuboresha huduma.
Uwekezaji wa boti hizo unatarajiwa kuleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za chanjo nchini, hasa katika maeneo yenye changamoto za kufikika, na hivyo kuimarisha afya ya jamii kwa ujumla.





