Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Mwenyekiti wa AAPAM Tawi la Tanzania (AFRICAN ASSOCIATION FOR PUBLIC ADMINISTRATION AND MANAGEMENT TANZANIA CHAPTER) Jumuiya ya Wataalamu wa Utawala wa Umma na Usimamizi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma barani Afrika Tawi la Tanzania, Bi. Leila Mavika, amesema kuwa AAPAM Tanzania kwa kushirikiana na jumuiya nyingine za wataalam wa utawala wa umma na usimamizi wa rasilimali watu, imeandaa mkutano mkuu wa pili wa mwaka utakaofanyika kuanzia Mei 5 hadi Mei 8, 2026.
Amesema kuwa mkutano huo unahusisha Tanzania Association for Public Administration and Human Resource (TAPAICHARA) pamoja na mtandao wa mameneja wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu Tanzania (TPSHRA-IMNET), ambao wameungana katika kuandaa mkutano huo muhimu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Aprili 29,2026, Jijini Dodoma, Bi. Leila Mavika, amebainisha kuwa mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kufikiria upya utoaji wa huduma kwa umma, matumizi ya teknolojia katika kuanzisha huduma bora na zinazolenga wananchi, kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na changamoto za mazingira.”
Ameongeza kuwa mkutano huo unalenga kuwakutanisha wataalam wa utawala wa umma na usimamizi wa rasilimali watu ili kujadili namna bora ya kuimarisha utawala, kubaini fursa zilizopo, kuimarisha ushirikiano wa wadau mbalimbali pamoja na kutatua changamoto zinazoathiri utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.
Amesema kuwa mkutano huo pia utajumuisha mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wataalam nguli katika utumishi wa umma watakaoshiriki kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi wa kazi.
Aidha amebainisha kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge.
Ameongeza kuwa katika siku ya mwisho ya mkutano, Mei 8, 2026, washiriki watapata fursa ya kufanya zoezi la kuimarisha ushirikiano wa kazi (team building) katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Kwa upande wake, Teophory Mbilinyi, mjumbe wa kamati tendaji ya (TPSHRA-IMNET) Chama kidogo ndani ya AAPAM, amesema kuwa kaulimbiu ya mkutano huo inagusa maeneo makubwa manne ambayo ni utoaji wa huduma bora kwa wananchi, matumizi ya teknolojia, ajira kwa vijana na masuala ya mazingira.
Amesema kuwa maeneo hayo ni muhimu na yanalingana na mwelekeo wa sasa wa serikali katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa wataalam wa rasilimali watu na utawala wana jukumu la kuhakikisha wanasimamia watumishi ipasavyo ili kuongeza tija na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wakati wote.
Aidha amebainisha kuwa mkutano huo utatoa nafasi ya kujadili mada muhimu pamoja na kupata uzoefu kutoka kwa wageni mbalimbali kutoka nchi za Afrika, jambo litakalosaidia kubadilishana ujuzi na kuboresha mifumo ya utendaji kazi.

