Wamiliki wa ardhi wametakiwa kulinda ardhi wanayoimiliki ili kuepuka migogoro ya ardhi na kuongeza usalama wa umiliki.
Akizungumza mjini Njombe Aprili 27 katika viwanja vya Mjimwema, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Njombe, Bw. Fulgence Kanuti, amesema kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda rasilimali ya ardhi.
Akigeukia zoezi la uhamasishaji ulipaji Kodi ya pango la ardhi, ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, kila mwananchi anayemiliki ardhi iliyopimwa anatakiwa kulipa kodi ya ardhi.
Amesema, serikali inaendelea na zoezi la kupima vipande vya ardhi ili kuhakikisha kila mmiliki anahusishwa katika mfumo rasmi wa ulipaji kodi.
“Faida za kumiliki ardhi kihalali ni pamoja na uwezo wa kukopesheka kirahisi, kuimarika kwa usalama wa milki, pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi,” amesema Bw. Kanuti.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Maendeleo ya Ardhi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bw Emanuel Amos amesema kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza mwamko kwa wananchi wa Wilaya ya Njombe kuhusu masuala ya ardhi.
Amesema, kutokana na hali hiyo, wizara kwa kushirikiana na halmashauri inaendelea kuendesha Kliniki za Ardhi mara kwa mara ili kutoa elimu kwa wananchi.
“Tunawahimiza wananchi kufika katika viwanja vya Mjimwema ili waweze kupata elimu sahihi kuhusu upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi,” amesema.





