*“Ili kufikia malengo ya Dira 2050 ni lazima sisi tukiwa washauri wa kisheria tukimbie mbele zaidi”- Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema kuwa Serikali iko mbioni kufanya maboresho ya sheria mbalimbali ili ziende sambamba na malengo ya Dira Taifa 2050.
Dkt. Homera ametoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2026 Jijini Arusha.
*“Nimpongeze Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameanza vizuri na sasa tunaenda kurekebisha sheria mbalimbali ili ziweze kueandana na malengo ya kufikia Dira ya 2050”.*
Akizungumza katika Mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria ameeleza kuwa ni muhimu kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kujiendeleza kitaalamu na Kimaarifa ili waweze kuishauri vizuri Serikali na kuinua uchumi wa Taifa.
*“Napenda kutoa rai kwenu mzidi kujiendeleza kitaaluma na kimaarifa ili muweze kulishauri vizuri Taifa letu hasa juu ya Sheria zipi zinapaswa kutungwa na kurekebisha kwa ajili ya kuchochea vizuri ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kweli kwa Wananchi wote.”* Amesema Dkt. Homera
Aidha, Dkt. Homera amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Menejimenti ya Ofisi kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*“Nimshukuru Mhe. Rais kwa kukuteua tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaitendea haki nafasi hiyo, pia nikupongeze Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yako kwa maboresho makubwa uliyoyafanya katika Ofisi hii.”* Amesema Mhe. Dkt. Homera.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari akizungumza awali kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, amesema kuwa ili kufikia malengo ya Dira 2050 ni muhimu kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakaongeza kasi katika maboresho ya Sheria mbalimbali.
*“Wakati wenzetu wengine wanakuja, wakute tayari tumezifungamanisha sheria zetu na malengo ya Dira 2050 kwa kuzifanya rafiki na wezeshi kwa sekta na malengo mbalimbali.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Katika hatua nyingine, Mhe. Johari amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna anavyoiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
*“Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitarudia tena kumshukuru, kwa dhati kabisa ya moyo wangu, Rais wa Nchi yetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Serikali yake imewezesha hayo kufanyika. Asante sana Mhe. Rais.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali .
Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewasisitiza Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia Nidhamu, Weledi na Uadilifu ili kuweza kufikia malengo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Taifa kwa ujumla.
*“Ni lazima kila mmoja wetu ajenge na kudumisha utamaduni wa uwajibikaji unaozingatia weledi, ubunifu katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.”* Amesema Mhe. Johari.
Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno amewaeleza Watumishi juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya mifumo mbalimbali ya TEHEMA iliyoko katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuwawezesha katika kutekeleza majukumu yao kwa haraka na urahisi.
*“Niwasisitize Watumishi juu ya matumizi ya Mifumo mbalimbali tuliyonayo kupitia mifumo hii tutaweza kutekeleza majukumu yetu kwa urahisi na ufanisi.”* Amesema Mhe. Maneno
Mkutano wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Watumishi wa Ofisi, umehusisha wasilisho kuhusu mafanikio ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taarifa ya Utendaji kazi ya mwaka 2023/2024, 2025/2026 na mpango wa bajeti 2026/2027, Mpango Mkakati wa Ofisi,Muundo mpya wa Ofisi, Uzinduzi wa Tovuti ya Ofisi, Mifumo ya TEHAMA, Blueprint, Kipeperushi cha Je Wajua, pamoja na vitabu vinne vya Risk Management Framework, Risk Register, Risk Fraud Management Framework na Risk Fraud Register.




