Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya kilimo nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya wakulima na uchumi wa Taifa.
Ameyasema hayo Aprili 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, amebainisha kuwa bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.19 mwaka 2025/2026. Amesema hatua hiyo inaonesha kuwa Serikali imeifanya sekta ya kilimo kuwa kipaumbele kikuu katika kukuza uchumi na ajira.
Pia amesema kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 17,148,290 mwaka 2021/2022 hadi tani 23,783,128 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 38.69.
Ameongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka tani 973,436 mwaka 2021/2022 hadi tani 1,596,311.18 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 63.99.
Aidha, amesema kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi imeongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi Dola za Marekani Bilioni 3.73 mwaka 2024/2025.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika ruzuku za pembejeo, umwagiliaji, masoko ya mazao na programu ya Building Better Tomorrow (BBT) kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuwainua vijana katika sekta ya kilimo.




