NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa Kheri James amezindua rasmi msimu wa tano wa mbio za Great Ruaha Marathon yenye kauli mbiu ‘Vibe Kitalii’ katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi binafsi, wadau wa uhifadhi, pamoja na wananchi kutoka ndani na nje ya mkoa huo.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa umeashiria mwanzo wa maandalizi ya tukio hilo kubwa la michezo na utalii linalofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa aliwashukuru wananchi na wadau wote kwa kujitokeza na kushiriki katika tukio hilo muhimu, akieleza kuwa ni ishara ya mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuendeleza sekta ya utalii, michezo na uchumi wa mkoa wa Iringa.
Alisisitiza kuwa Great Ruaha Marathon si tukio la kawaida bali ni jukwaa linalounganisha sekta mbalimbali ikiwemo utalii, afya, uhifadhi wa mazingira, michezo na biashara.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka iliyopita, mbio hizo zimekua kwa kasi na kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, hali inayochochea ongezeko la fursa za ajira, biashara na uwekezaji kwa wananchi wa Iringa. Kwa mwaka 2026, inatarajiwa kuwa na zaidi ya washiriki elfu moja mia mbili jambo linalodhihirisha umaarufu na kukua kwa tukio hilo kimataifa.
Mbio hizo zitahusisha vipengele mbalimbali ikiwemo kilometa 5, kilometa 10 na kilometa 21, pamoja na shughuli nyingine kama vile uvuvi wa michezo, matembezi ya utalii (walking safari) na safari za baiskeli.
Shughuli hizo zitafanyika ndani ya mazingira ya kipekee ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, zikitoa fursa kwa washiriki kufurahia vivutio vya asili.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa serikali imeendelea kuboresha miundombinu muhimu ili kurahisisha shughuli za utalii katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara zinazoelekea hifadhini, pamoja na kuboreshwa kwa usafiri wa anga katika eneo hilo.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya utalii kwa kuwekeza katika huduma za malazi, usafiri na biashara nyingine zinazohusiana na wageni.
Pia alisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira, hususan vyanzo vya maji, ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) Eward Milinga
alieleza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na kubainisha mafanikio yaliyopatikana katika misimu iliyopita, ikiwemo kuongezeka kwa watalii, kuimarika kwa juhudi za uhifadhi na kukuza vipaji vya michezo kwa vijana.
Aliongeza kuwa mwaka huu wameongeza kipengele cha mbio za baiskeli ili kuongeza ushiriki na ubunifu.
Vilevile, alitoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kikamilifu katika kufanikisha tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kusaidia katika uhamasishaji, matangazo na utoaji wa huduma kwa wageni watakaohudhuria.
Aliomba pia mamlaka husika kuruhusu upambaji wa jiji kwa mabango ya matangazo ili kuongeza uelewa wa tukio hilo kwa wananchi.
Great Ruaha Marathon inatarajiwa kufanyika mwezi Julai 2026, huku kilele cha mbio kikipangwa kuwa siku maalum ambapo washiriki watashindana katika vipengele mbalimbali vya mbio.
Tukio hilo linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.
Mratibu wa mbio hizo, Hamim Kilahama, amesema kuwa Great Ruaha Marathon inalenga kutangaza utalii wa nyanda za juu kusini na kuhamasisha utunzaji wa mazingira, hususan uhifadhi wa Mto Ruaha ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa taifa zima.
Mkuu wa Mkoa aliwahakikishia wageni wote usalama wa hali ya juu wakati wote wa tukio, akisisitiza kuwa serikali ya mkoa imejipanga kikamilifu kuhakikishak mbio hizo zinafanyika kwa mafanikio makubwa. Alitoa wito kwa Watanzania na wageni wa kimataifa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushuhudia uzuri wa tukio hilo la kipekee.





