Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo akizungumza kwenye hafla hiyo jijini Arusha .
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, amekabidhi rasmi magari mawili mapya pamoja na mfumo wa matangazo (PA System) kwa watumishi wa Jiji la Arusha.
Aidha kutolewa kwa magari hayo ni mojawapo ya juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi
Vifaa hivyo vimenunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani ya jiji, jambo linaloonyesha uwezo wa halmashauri kujitegemea kifedha na kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wake.
“Hatua hii ni sehemu ya mikakati ya jiji katika kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora, za haraka na zenye ufanisi mkubwa.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa jiji la.Arusha Kayombo amesema kuwa upatikanaji wa magari hayo pamoja na mfumo wa matangazo utasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kila siku, ikiwemo shughuli za ukusanyaji wa mapato, ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa taarifa kwa umma kwa wakati.
Aidha, amewataka watumishi waliokabidhiwa vifaa hivyo kuhakikisha wanavitunza kwa uangalifu na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa jiji pamoja na wananchi wake kwa ujumla.
Kwa upande wao, baadhi ya watumishi waliopokea vifaa hivyo wameishukuru menejimenti ya jiji kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi, wakiahidi kuvitumia kwa ufanisi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Zoezi hilo la makabidhiano limefanyika katika viwanja vya Jiji la Arusha, likihudhuriwa na watumishi mbalimbali pamoja na viongozi wa jiji hilo




