Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya Men at Work Global ieweka mkakati wa miaka 10 ijayo ya kujenga kituo maalumu kwaajili ya kutoa mafunzo kwa watoto na vijana wa kiume hatua itakayosaida kuandaa wanaume bora watakaokuwa na uwezo wa kujitambua,kujisimamia na kuhudumia familia zao kikamilifu.
Hayo yamebainishwa Aprili 26, 2026 na Rais wa taasisi hiyo, Maxwell Shing’oma kwenye kongamano la wanaume lililofanyika jijini Mwanza.
Amesema malezi bora kwa watoto ndio msingi pekee ambao utamuwezesha kuwa mwanaume bora kuanzia kwenye familia,jamii na taifa kwaujumla.
Aidha, amewakumbusha wazazi na walezi kuwajibika ipasavyo katika malezi na makiluzi ya watoto wao,huku akisisitiza kituo hicho kitakuwa cha mfano katika kuwasaidia watoto wakiume kujitambua.
“Tunaiomba serikali itusaidie tupate eneo kwaajili ya kujenga kituo hicho ili shule zinapofungwa watoto wakiume waweze kufika kwenye kituo kwaajili ya kupata elimu”,
Kwaupande wake Mwalimu wa Stadi za Maisha kutoka Taasisi ya Hekima Talk, Timothy Kyara amewataka wanaume nchini kujenga na kulinda majina yao kwa hasira kubwa huku pia akihimiza umuhimu wa kuanzisha mifumo imara ya fedha itakayowawezesha kujitegemea kiuchumi hata wanapokuwa hawafanyi kazi moja kwa moja.
“Mwanaume linda kwa hasira jina lako kuna mambo hutafanya kwa sababu unalinda jina lako, kuna watu hutakuwa karibu nao kwa sababu unalinda jina lako ukifika mahali likitajwa jina lako lina maanisha kitu, kuna majina ukitaja milango inafunguka,” amesema
Hata hivyo Kyara amewataka wanaume kuanzisha na kutengeneza mifumo ya kipato endelevu badala ya kutegemea kipato cha muda mfupi ili kutokuyumba kiuchumi kipindi amepata shida au wakati wa uzeeni.




