Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn Boshe akifungua jukwaa la kikanda lililofanyika katika makao makuu ya African Union jijini Addis Ababa,Ethiopia Aprili 27, 2026.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Kadari Singo akizungumza katika jukwaa la kikanda lililofanyika katika makao makuu ya African Union jijini Addis Ababa,Ethiopia Aprili 27, 2026.
……………
Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn Boshe, amesema Afrika inapaswa kuchukua hatua za kimkakati ili kuondokana na utegemezi wa kusafirisha malighafi nje ya bara na badala yake kuhakikisha madini yake yanaongezewa thamani ndani ya Afrika kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati akifungua jukwaa la kikanda lililofanyika katika makao makuu ya African Union jijini Addis Ababa, alisema madini muhimu kama kobalti, lithiamu, shaba, manganisi na madini adimu ndiyo msingi wa mapinduzi ya viwanda vya kijani duniani.
Alieleza kuwa madini hayo yana mchango mkubwa katika utengenezaji wa betri, magari ya umeme na mifumo ya nishati jadidifu, lakini akasisitiza kuwa Afrika bado haijafaidika ipasavyo licha ya kuwa na akiba kubwa ya rasilimali hizo.
Boshe alionya kuwa hali ya wananchi wa Afrika kuendelea kuwa maskini huku wakimiliki utajiri mkubwa wa rasilimali haiwezi kuendelea, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kijani yanapaswa kuwa chachu ya maendeleo na si “uchimbaji bila mabadiliko.”
Alisisitiza kuwa Afrika inapaswa kuacha nafasi ya kuwa msafirishaji wa malighafi na badala yake kujenga uwezo wa viwanda vya ndani vinavyoweza kuchakata na kuongeza thamani ya rasilimali zake.
Alieleza kuwa hatua hiyo ndiyo itakayowezesha bara hilo kunufaika kikamilifu na rasilimali zake.
Katika kufanikisha hilo, alitoa wito wa kuanzishwa kwa mitambo ya kusafisha na kuchakata madini, viwanda vya betri na vifaa vya nishati, pamoja na viwanda vya chuma na alumini vinavyotumia nishati ya kijani ili kuhakikisha ukuaji wa viwanda unakuwa endelevu.
Pia alisisitiza umuhimu wa miundombinu imara na uwekezaji katika nishati jadidifu kama jua, upepo na jotoardhi, akieleza kuwa viwanda haviwezi kustawi bila mfumo thabiti wa nishati na usafirishaji wa kisasa.
Alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda kupitia African Continental Free Trade Area, akibainisha kuwa nchi za Afrika zikishirikiana zinaweza kujenga minyororo ya thamani yenye ushindani wa kimataifa na kuimarisha uchumi wa bara.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Kadari Singo, alisema Afrika inaongeza juhudi za kuhakikisha madini yake muhimu yanachangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi kupitia viwanda vya kijani na kuongeza thamani ndani ya bara.
Alieleza kuwa wakati mahitaji ya kimataifa ya madini ya nishati safi yakiendelea kuongezeka, Afrika ina fursa ya kipekee ya kujipanga katika minyororo ya thamani ya kimataifa, lakini mafanikio yake yanategemea sera thabiti, utawala bora na ushirikiano wa pamoja.
Singo alisema jukwaa hilo limewakutanisha watunga sera, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kujadili namna bora ya kuongeza thamani ya madini ndani ya Afrika, kwa lengo la kuimarisha viwanda vya ndani na kukuza uchumi jumuishi.
Alibainisha kuwa majadiliano yamejikita katika kuwekeza kwenye viwanda vya ndani, kukuza ujuzi na kuboresha mifumo ya usimamizi wa rasilimali ili kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa nchi za Afrika.
Aidha, alisisitiza kuwa Taasisi ya UONGOZI itaendelea kusaidia serikali kupitia tafiti, majadiliano ya sera na programu za maendeleo ya uongozi kwa lengo la kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali asilia.
Singo alihitimisha kwa kueleza kuwa jukwaa hilo ni hatua muhimu kuelekea mkutano mkubwa wa bara kuhusu maendeleo endelevu, ambapo matarajio ni kupata mapendekezo yatakayosaidia Afrika kutumia madini yake kwa ufanisi zaidi na kujenga uchumi endelevu wa muda mrefu.

