Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
Mwenge wa Uhuru umeonesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi saba wilayani Rufiji mkoani Pwani, ukiwemo mradi wa barabara ya Chumbi–Kiegele unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wenye thamani ya shilingi bilioni 1.499.
Mradi huo wenye urefu wa kilometa 8, ambapo kilometa 1.1 zimejengwa kwa kiwango cha lami, unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi pamoja na kuunganisha maeneo ya wilaya hiyo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, aliridhishwa na utekelezaji wake na kuwataka wananchi kuutunza.
Katika mtandao wa barabara wilaya ya Rufiji ina jumla ya kilometa 523.51 kati ya hizo kilometa 14.281 ni za lami, kilometa 78.14 ni changarawe na kilometa 431.089 ni udongo.
Kadhalika Mwenge wa Uhuru umekagua mradi wa maji kijiji cha Ndundutawa wenye thamani ya shilingi milioni 207.269, ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na ofisi mbili za walimu katika Shule ya Sekondari Bwawani, na mradi wa ranchi ndogo kijiji cha Chumbi C na ugawaji wa hati kwa wafugaji Kata ya Chumbi.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zimefikia siku ya tisa mkoani Pwani tangu ulipopokelewa Aprili 18, 2026, na zinatarajiwa kuhitimishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kabla ya kukabidhiwa mkoani Lindi Aprili 27, 2026.





