Na Mwandishi Wetu
PWANI, Aprili 26, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewahimiza wananchi wa mkoa huo pamoja na Watanzania kwa ujumla kuendelea kupanda miti kwa wingi na kuepuka ukataji holela, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kunenge alitoa kauli hiyo leo Aprili 26,2026 wakati wa maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yaliyofanyika katika Hospitali ya Lulanzi, Kibaha, ambapo alisema juhudi za upandaji miti zinaunga mkono sera na maelekezo ya Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi za kupikia.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatunza mazingira kwa vitendo. Kupanda miti si tu kunasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, bali pia kunaboresha afya na ustawi wa jamii,” alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Pwani utaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji miti pamoja na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa unaochangia uharibifu wa misitu.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mkama Kusaga, aliyemwakilisha Kamanda wa Kanda ya Mashariki, alisema jumla ya miche 600 imepandwa katika eneo la Hospitali ya Lulanzi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono uhifadhi wa mazingira.
“Upandaji huu wa miti ni mwendelezo wa utekelezaji wa sera ya taifa ya utunzaji wa mazingira pamoja na kuhamasisha matumizi bora ya nishati safi ya kupikia kama gesi,” alisema Kusaga.
Maadhimisho hayo ya miaka 62 ya Muungano yamekuwa jukwaa muhimu la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda rasilimali za asili na kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto za kimazingira.





