‎Na. John Bukuku- Dar es salaam

‎Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuungana kwa pamoja kulirejesha taifa kwenye misingi yake, huku akieleza kuwa serikali itachukua hatua za haraka kufuatia mapendekezo ya taarifa ya tume.

‎Ameyabainisha hayo Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, akisema kuwa katika muda mfupi ujao itaundwa tume ya maridhiano itakayojumuisha wadau wote muhimu kwa ajili ya kusimamia na kuongoza majadiliano na maridhiano ili kuziba mianya na migawanyiko iliyopo na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa.

‎Aidha, amebainisha kuwa kabla ya kuundwa kwa tume hiyo, serikali itakwenda kwenye mapendekezo ya tume kufanya upelelezi wa kina wa mambo yaliyobainishwa.

‎Pia amesema kuwa nia ya kuunda tume ya maridhiano ilikuwepo hata kabla ya matukio ya Oktoba 25 na ilikuwa ni miongoni mwa ahadi zake za siku mia za kwanza, lakini utekelezaji wake umecheleweshwa na ghasia zilizotokea.

‎Ameongeza kuwa hadidu za rejea za tume hiyo zitapaswa kubadilika ili kuendana na mazingira yaliyopo sasa.

‎Aidha, amebainisha kuwa baada ya tume ya maridhiano kuwasilisha ripoti yake, maoni na mapendekezo yatakayotolewa yataelekeza mchakato wa kurekebisha Katiba ya nchi.

‎Pia ameongeza kuwa kutokana na ripoti kubainisha kuwepo kwa viashiria vya jinai, serikali itaunda chombo maalum cha upelelezi kwa ajili ya kufanya kazi iliyopendekezwa na tume.

‎Aidha, amebainisha kuwa chombo hicho kitachunguza na kubaini waliohusika katika kupanga, kuratibu na kufadhili matukio ya ghasia au vurugu, pamoja na kubaini wahusika wa matukio ya uhalifu yaliyotokea.