Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 23 Aprili, 2026.
………….
Na John Bukuku – Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ujenzi wa demokrasia unapaswa kuzingatia mila na tamaduni za nchi husika, akinukuu kauli ya Baba wa Taifa Julius Nyerere kwamba demokrasia si jambo la kuagizwa kama bidhaa.
Pia ameongeza kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kujenga demokrasia yake kwa misingi yake, akieleza kuwa kupitia falsafa ya 4R alichukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha majadiliano na wadau wa siasa yaliyopelekea marekebisho ya baadhi ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa. Ameongeza kuwa hatua hizo zimeenda sambamba na kupanua wigo wa shughuli za kisiasa pamoja na kukuza uhuru wa vyombo vya habari.
Ameyabainisha hayo Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, akisema kuwa tangu kupata uhuru na baada ya Muungano, Tanzania ilichagua kufuata mfumo wa demokrasia, na mwaka 1992 ikaingia katika mfumo wa vyama vingi. Aidha, amebainisha kuwa kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, demokrasia inapaswa kuendelezwa kulingana na mazingira ya nchi yenyewe badala ya kuiga mifumo ya nje.
Aidha, Rais Samia amesema kuwa ni rahisi kupoteza amani lakini si rahisi kuirejesha, na kwamba kubomoa nchi ni jambo rahisi kuliko kuijenga. Amebainisha kuwa changamoto katika maendeleo hazikwepeki, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika kuzitatua badala ya kuzigeuza kuwa chanzo cha vurugu na uhalifu.
Pia ameongeza kuwa matukio yaliyotokea hayakuondoa changamoto zilizokuwepo bali yalizidisha, hivyo amesisitiza umuhimu wa Watanzania kulinda amani na kushiriki katika ujenzi wa taifa. Amesema kuwa Watanzania ndio msingi wa ujenzi wa nchi na hakuna msaada wa nje utakaoweza kuisaidia nchi endapo itachagua kuharibu misingi yake.
Aidha, amebainisha kuwa baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, kulikuwepo na taarifa mbalimbali zilizotolewa bila usahihi, ikiwemo takwimu za vifo zilizokuwa hazijathibitishwa. Amesema kuwa baadhi ya taarifa hizo zilikuwa na lengo la kupunguza au kuongeza ukubwa wa madhara yaliyotokea.
Pia ameongeza kuwa Tume ya uchunguzi imewasilisha takwimu sahihi baada ya kufanya uchambuzi wa kitaalamu, zikionesha idadi ya waliopoteza maisha, waliojeruhiwa na waliopata madhara mengine. Ameeleza kuwa madai ya wananchi kuhusu ndugu zao kutoweka yataendelea kuchunguzwa kwa kina ili kubaini ukweli wake.





