Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCD), Dkt. Benson Ndiege akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Aprili 22, 2026 kuhusu mkutano wa wadau wa ushirika na uzinduzi wa kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” unaolenga kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika vyama vya ushirika nchini.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCD), Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa serikali imeandaa mkutano wa wadau wa ushirika kwa lengo la kujadili hali ya sekta na mikakati ya kukabiliana na changamoto ya uadilifu katika uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini.
Amesema kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kulinda maslahi ya wanachama na kujenga imani kwa wadau wa ushirika, ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa chombo imara cha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Ameyabinisha hayo Aprili 22,2026, Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari.
Aidha, amebainisha kuwa pamoja na mkutano huo, serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika itazindua kampeni maalum yenye kaulimbiu “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji, haki na utawala bora katika vyama vya ushirika.
Pia amesema kuwa Tume imepewa jukumu la kusimamia maendeleo ya ushirika nchini, ikiwemo kuhamasisha wananchi kuhusu fursa zilizopo na kuhakikisha vyama vilivyosajiliwa vinafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.
Ameongeza kuwa baadhi ya vyama vya ushirika vinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wizi, ubadhirifu na usimamizi usioridhisha, hali inayohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kukabiliana nayo.
Aidha, amebainisha kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume hufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali na kuziwasilisha kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi za kisheria.
Huku akibainisha kuwa ushiriki wa wadau wote ni muhimu ili kuhakikisha juhudi za kuimarisha uadilifu katika sekta ya ushirika zinafanikiwa.
Mkutano huo utafanyika Aprili 24, 2026 katika Ukumbi wa PSSF jijini Dodoma, ukitarajiwa kuwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo wanachama wa vyama vya ushirika, viongozi, taasisi za haki, viongozi wa serikali, wanasiasa, watoa huduma pamoja na vyombo vya habari huku Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo.




