Farida Mangube Sikonge, Tabora
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Thomas Mnyinga amewataka wakazi wa wilaya hiyo kulinda na kuhifadhi misitu ya miombo, akieleza kuwa rasilimali hiyo imeanza kuwa kivutio muhimu cha utalii na inaweza kuchangia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Akizungumza katika Tamasha la Staff Tour 2026 lililofanyika ndani ya hifadhi ya msitu wa mazingira Itulu hills na kubebwa na kauli mbiu “Tunaungana, Tunaitunza, Tunaburudika na Miombo,” Mkuu huyo wa Wilaya alisema ni muhimu kwa jamii kubadili mtazamo na kuitunza misitu hiyo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Alisema pamoja na umuhimu wa miombo, bado kuna matumizi makubwa ya miti hiyo, hususan katika ukaushaji wa tumbaku ambapo wakulima hutumia kuni kwa wingi.
“Serikali ipo katika mpango wa kuleta mbadala wa kukaushia tumbaku ili kupunguza matumizi ya kuni na kulinda misitu yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa uhifadhi wa misitu hiyo utasaidia kukuza utalii wa mazingira, ambao unaanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Miongoni mwa vivutio vilivyotajwa ni Mto Koga, ambao unatenganisha mikoa ya Tabora na Katavi. Mto huo umeelezwa kuwa na uhai wa viumbe mbalimbali wakiwemo viboko wanaoonekana katika baadhi ya maeneo.
Aidha, ndege wa aina mbalimbali huonekana katika eneo la mto huo wakifika kutafuta chakula, hali inayoongeza mvuto kwa watalii wanaopenda kutazama wanyamapori na ndege.
Akizungumzia tamasha hilo, Afisa Utalii kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Sikonge Mhifadhi John Shayo alisema lengo ni kuhamasisha utalii wa miombo na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu hiyo yenye bioanuai kubwa.
“Tunataka jamii itambue kuwa misitu hii ina thamani zaidi ya matumizi ya kawaida, ikiwemo fursa za utalii,” alisema.
Mbali na shughuli za utalii wa asili, washiriki wa tamasha hilo pia walipata fursa ya kufurahia burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili pamoja na vyakula mbalimbali ikiwemo nyama choma.
Tamasha hilo limeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kukuza utalii wa ndani huku likihamasisha uhifadhi wa rasilimali misitu katika Wilaya ya Sikonge.







