Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amewahimiza vijana nchini kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili kujikwamua kiuchumi.
Mwang’onda alitoa rai hiyo Aprili 20, 2026 alipokuwa akikagua mradi wa kikundi cha vijana watano walioanzisha Zahanati ya Mujore, iliyopo Kata ya Kawawa, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Zahanati hiyo inajishughulisha na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Imeelezwa lengo la kikundi hicho ni kujiajiri pamoja na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hali inayopunguza gharama kubwa za usafi
ri kwa wanaohitaji matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa, kikundi hicho kilipatiwa mkopo wa halmashauri katika awamu mbili; mwaka wa fedha 2024/2025 kilipata Sh milioni 30 na mwaka 2025/2026 kilipata mkopo mwingine wa Sh milioni 30 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Zahanati hiyo imetoa ajira kwa vijana wengine saba na hadi sasa imeshahudumia wananchi zaidi ya 4,800.
Mwang’onda alisifu juhudi za vijana hao, akieleza kuwa wanafanya kazi kubwa katika jamii.
Vilevile, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza utoaji wa fedha katika halmashauri, pamoja na kusisitiza ukusanyaji wa mapato ya ndani unaowezesha kutengwa kwa asilimia 10 kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwaunga mkono vijana hao kwa kutumia huduma zinazotolewa katika zahanati hiyo.
April 21 mwenge wa Uhuru utakuwa Manispaa ya Kibaha ukitokea halmashauri ya wilaya ya Kibaha.





