Halmashauri ya Mji wa Kasulu ni miongoni mwa halmashauri 45 za miji nchini zitakazonufaika na Mradi wa TACTIC baada ya kutengewa shilingi bilioni 10.87 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maendeleo ya mijini.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, aliyetaka kujua lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za Kasulu – Kigondo na Habitat – Hwazi kupitia mradi huo.
Akijibu swali hilo Mhe. Dkt. Dugange amesema tayari usanifu wa miradi hiyo umekamilika na maandalizi ya kuanza utekelezaji yanaendelea kwa kushirikiana na World Bank.
“Mradi wa TACTIC umekamilisha usanifu wa miradi ya Mji wa Kasulu wa barabara za Makaburi–Kigondo km 3.77, Habitat–Hwazi km 2.04, jumla ya km 5.8. Mradi huu utahusisha pia ujenzi wa stendi ya mabasi ya Murus na soko la Kumsenga Kasulu,” amesema Dkt. Dugange.
Aidha, Dkt. Dugange amefafanua kuwa Kasulu ipo katika kundi la tatu la utekelezaji wa mradi huo linalojumuisha miji 18 nchini, hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kurahisisha usafiri na usafirishaji pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo.






