Katikati aliyevaa tracksuit nyeusi kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Katavi Sipha Mwanjala akishiriki katika mazoezi ya viungo.
20.04.2026
Na mwandishi wetu, Mlele
Wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi wamefanya bonanza kubwa la michezo lililoandaliwa na ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa mkoa a Katavi likiwa na lengo la kuendelea kutoa elimu ya kupinga vitendo vya rushwa katika maeneo mbalimbali hususan michezo.
Akifungua bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya michezo vya shule ya msingi Inyonga Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga amesisitiza ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali na TAKUKURU.
Mkuu huyo wa wilaya Mlele alisema ushirikiano baina ya taasisi na makundi mbalimbali ya kijamii kama vijana, wanawake, waendesha boda boda n.k unawezesha serikali kutekeleza kazi zake kwa urahisi huku wananchi wakiwa na amani ya kutosha.
Ameongeza kuwa michezo inaimarisha afya ya mwili na akili na kuwashukuru TAKUKURU kwa kufanya bonanza hilo katika wilaya yake.
Katika bonanza hilo vijana wanaoendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda waligaiwa vizibao maalum vyenye ujumbe wa kukataa rushwa.
Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Katavi Bi. Sipha Mwanjala alisema lengo la bonanza hilo ni kushirikiana na wadau mbalimbali katika michezo na kutoa elimu ya rushwa.
“Tunaamini kwamba mtu akifanya mazoezi ataepukana na magonjwa yasiyo ya kumbukiza, na atachapa kazi kwa bidii” alisema Bi. Mwanjala.
Bonanza hilo lilinogeshwa na michezo mbalimbali ikiwemo bao, draft, mpira wa miguu, sarakasi, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kukimbia na magunia, riadha, kushindana kupanga soda kwenye kreti, kushindana kula kupitia kisinia baada ya kurusha chupa, na kutembea na yai kwenye kijiko.
Naye Afisa Michezo wa halmashauri ya Mlele Godfrey Uisso alisema mbinu waliyotumia TAKUKURU kufikisha ujumbe wa kupinga rushwa ni nzuri kwani imekutanisha makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi ambao nao ni mabalozi wazuri katika kufikisha ujumbe kwa jamii.




